Wednesday, September 7, 2022

BAKITA YATOA VITABU 1,650 VYA KISWAHILI KWA UBALOZI WA TANZANIA UJERUMANI

Katika jitihada za kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili Duniani Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limetoa vitabu 1,650 vya Kiswahili  vitakavyotumiwa na vyuo, vituo na taasisi zinazojishughulisha na ufundishaji wa lugha ya Kiswahili nchini  Ujerumani.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vitabu hivyo, iliyofanyika jijini Dar es Salaam,  Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine ameipongeza BAKITA kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya katika kubidhaisha lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Kimataifa.

“Naamini kuwa BAKITA itaendelea kufungua mlango kwa ajili ya maombi ya vitabu vya kufundishia lugha ya Kiswahili katika nchi rafiki na nchi nyingine zote duniani ambazo zitaonesha nia ya kufundisha raia wake lugha adhimu ya Kiswahili, alisema Balozi Sokoine

Alisema kuwa juhudi hizo ni muhimu sana wakati huu kwa kuwa Shirika la UNESCO liliipitisha tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani, huku SADC, EAC na AU pia zilipitisha lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika katika utendaji kazi wa mitangamano hii na kuongeza kuwa kwa sasa ni dhahiri kuwa lugha ya kiswahili itakuwa kwa kasi na mahitaji ya vitabu na zana nyingine za kufundishia yataongezeka pia

"Kitendo hiki ni muhimu sana hasa ikizingatiwa kuwa  UNESCO iliipitisha tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani, SADC, EAC na AU nazo zilipitisha lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi za kazi, ni dhahiri kuwa lugha hii sasa itakuwa kwa kasi na hivyo, mahitaji ya vitabu na zana nyingine za kufundishia yataongezeka,” amesema Balozi Sokoine.

Naye Naibu katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema uchapishwaji wa vitabu hivyo utasaidia kukuza lugha ya kiswahili nchini Ujeremani pamoja na mataifa mengine ya jirani.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi. Consolata Mushi ameahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuendelea kubidhaisha lugha ya Kiswahili kimataifa zaidi.

“BAKITA katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria na mkakati wa taifa wa kubidhaisha Kiswahili itaendelea kusambaza vitabu katika balozi mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikiwemo Urusi, Uholanzi, Afrika Kusini, Burundi, Namibia, Korea Kusini, Nigeria na Mauritius,” amesema Bi. Mushi

Ameongeza kuwa BAKITA imetoa vitabu hivyo ikishirikiana na wachapishaji wa vitabu kutoka kampuni mbalimbali kwa lengo la kubidhaisha lugha ya Kiswahili na kutangaza soko jipya la vitabu katika nchi za Ulaya ikilenga kuwasaidia walimu wanaofundisha Kiswahili ambao ni Wadachi wenye nasaba na Waswahili pamoja na Diaspora wa Tanzania ambao wameanza kufundisha Kiswahili.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu wakimsikiliza Katibu Mtendaji wa (BAKITA), Bi. Consolata Mushi alipokuwa akitoa maelezo kuhusu ukumbi unaotumika kwa tafsiri za lugha mbalimbali katika taasisi hiyo

Katibu Mtendaji wa (BAKITA), Bi. Consolata Mushi akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya makabidhiano ya nakala 1,650 za vitabu vitakavyotumiwa na vyuo, vituo na taasisi zinazojishughulisha na lugha ya Kiswahili Ujerumani 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (katikati) akiwasilisha hotuba yake wakati wa hafla ya makabidhiano ya nakala 1,650 za vitabu vitakavyotumiwa na vyuo, vituo na taasisi zinazojishughulisha na lugha ya Kiswahili Ujerumani 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiangalia moja kati ya Vitabu vilivyotolewa na BAKITA kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani. Wengine ni Naibu katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (kulia) pamoja na Katibu Mtendaji wa (BAKITA), Bi. Consolata Mushi (kushoto)

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akipokea boksi la Vitabu vilivyotolewa na BAKITA kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani kutoka kwa Naibu katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu pamoja na Katibu Mtendaji wa (BAKITA), Bi. Consolata Mushi

Meza Kuu katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa BAKITA


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.