Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema takribani wawakilishi wa Kampuni 1,000 za nchini Italia wamethibitisha kushiriki kwenye Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji linalotarajiwa kufunguliwa rasmi jijini Zanzibar tarehe 28 Septemba 2022.
Akizungumza leo tarehe 27 Septemba 2022 jijini Zanzibar wakati wa mkutano wa maandalizi uliokuwakutanisha Wawekezaji na Wafanyabiashara kutoka Italia na Maafisa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoka Sekta zinazosimamia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Kombo amesema mwitikio huo mkubwa wa washiriki wa kongamano kutoka Italia unatokana na jitihada zinazofanywa na ubalozi katika kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na utalii nchini humo.
“Ubalozi wa Tanzania nchini Italia umeendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji, utalii na biashara zilizopo nchini. Ni kutokana na jitihada hizo Kampuni nyingi zimehamasika na kuonesha nia ya kuja kujionea fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zitakazowasilishwa wakati wa Kongamano hili. Nimefarijika sana kuona mwitikio huu wa washiriki kutoka Italia ambao umezidi ule wa kongamano la kwanza” amesema Balozi Kombo.
Kadhalika ameongeza kusema kuwa tayari zipo Kampuni kadhaa za Italia zimewekeza nchini ikiwemo ile ya Toscana Macchine Calzature (TMC) iliyopo mkoani Kilimanjaro inayojishughulisha na uuzaji wa mashine za kisasa na vipuri vyake vya utengenezaji wa viatu na bidhaa na ngozi. Amesema Kampuni hiyo ambayo huzalisha viatu zaidi ya jozi 4,000 kwa siku, imeonesha utayari wa kutoa wataalam saba (7) watakao toa mafunzo ya utengenezaji bidhaa za ngozi katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar.
Vilevile, Balozi Kombo ameeleza kuwa, kutokana na jitihada zinazofanywa na ubalozi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii hapa nchini safari za ndege za watalii kutoka Italia zimeongezeka kutoka safari tatu hadi nane kwa wiki.
Balozi Kombo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa za soko la bidhaa kama Parachichi ambazo tayari zimeanza kuuzwa nchini Italia.
Kwa upande wake, Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji na kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana Tanzania katika kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.
Kongamano hilo ambalo litafunguliwa rasmi tarehe 28 Septemba 2022, linalenga pamoja na mambo mengine kujadili kwa kina namna ya kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kupitia sekta ya biashara na uwekezaji. Pia kutoa nafasi kwa Tanzania kuainisha fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini zinazoweza kuchangamkiwa na washiriki kutoka Italia.
Kongamano hilo ambalo ni mwendelezo wa Kongamano la Kwanza la aina hii lililofanyika jijini Rome, Italia mwezi Desemba 2021, linatarajiwa kuhitimishwa jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2022.
Mhe. Balozi Lombardi akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi ya Kongamano la Pili la Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia |
Washiriki kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wawekezaji na Wafanyabiashara kutoka Italia wakati wa kikao baina yao |
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Bw. Sharif Ali Sharif akifuatilia kikao |
Kikao kikiendelea |
Kikao kikiendelea |
Sehemu ya Maafisa Waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakifuatilia kikao |
Afisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Salma Baraka akinukuu mazungumzo wakati wa kikao |
Kikao kikiendelea |
Mwekezaji kutoka Italia akizungumza wakati wa kikao |
Mwekezaji kutoka Italia akichangia jambo wakati wa kikao |
Picha ya pamoja |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.