Monday, September 26, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE YATOA WITO KWA WADAU KUFUNGUA HUDUMA MAALUM KWA DIASPORA


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekutanisha wadau wa sekta ya umma na  binafsi katika mkutano wa kujadili masuala ya diaspora na ushirikishwaji wao ili waweze kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ufanisi zaidi.

Akifungua mkutano huo  wa siku mbili tarehe 26 na 27 Septemba 2022, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agness Kayola ameeleza kuwa madhumuni ya mkutano  huo ni  kujadili namna wadau hao watakavyoweza kuongeza huduma za taasisi zao kwa diaspora ili kuleta ushirikiswaji wenye tija katika maendeleo ya Taifa.

“Mkutano huu umewakutanisha wadau wanaotoa huduma mbalimbali kwa Diaspora na wale ambao hawana huduma bado, lakini ni Wadau wanaoweza kuwa na mchango muhimu katika kuongeza ushiriki wa Diaspora wa Tanzania kwenye masuala ya maendeleo ya taifa’’ alisema Balozi Kayola.

Pia akaeleza kupitia mkutano huo wadau watapata fursa ya kushirikishana juu ya masuala mbalimbali muhimu, kama vile Fursa za Uwekezaji nchini; Vigezo vya Kusajili Wawekezaji Wazawa na Wawekezaji Wageni, wakiwemo Diaspora wenye Uraia wa nchi nyingine; Fursa za Uwekezaji kwa Diaspora na nini kifanyike kuongeza Uwekezaji kutoka kwa Diaspora wa Tanzania.

Naye Mkurugenzi wa masuala ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana ameeleza kuwa mkutano huo umezikutanisha taasisi za fedha, kampuni za simu za mikononi, taasisi za umma na binafsi za ujenzi wa nyumba za makazi kama vile Shirika la nyumba la Taifa (NHC), Hamidu City Park, KC Land na wengine.

Vilevile ameeleza kuwa kupitia mkutano huo Serikali na wadau wa sekta binafsi wataweza kujadili namna mataifa mengine duniani yalivyofanikiwa katika eneo la ushirikishwaji wa diaspora ikiwa ni hatua ya kuboresha huduma za sekta binafsi katika kuchagiza ari na hamasa ya diaspora kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

"Takwimu zinaonesha nchi kama China, India, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Ghana, Nigeria zilivyofanikiwa katika eneo la dispora hivyo, hatuna budi kuongeza ubunifu ili kufanikisha mikakati yetu ya kitaifa kwa kuunganisha nguvu ya diaspora na sekta binafsi" alisema Balozi Bwana.

Kwa upande wa Naibu Mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Diaspora, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Bi. Maryam Ramadhan Hamoud ameeleza kuwa mkutano huo utawafahamisha wadau kuhusiana na mchango wa Diaspora katika sekta mbalimbali hususan Afya, Elimu, Uwekezaji na umuhimu wa Diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia fedha wanazotuma nyumbani (Remittances).

Mbali na hayo Bi. Maryam aliongeza kuwa, wadau watapata fursa ya kutambua huduma mbalimbali za misaada ya kijamii, Sayansi na Ubunifu, ambayo huletwa nchini na Wafadhili kupitia uratibu wa Diaspora.

Mwaka 2010, Serikali ilianzisha Kitengo cha Diaspora chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilianzishwa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Masuala ya Diaspora katika Ofisi ya Rais Ikulu – Zanzibar. Jukumu kubwa la Ofisi hizi mbili, ni kusimamia, kuratibu na kushughulikia masuala yanayohusu Ushiriki wa Diaspora katika shughuli za Maendeleo ya nchini.
Mkurugenzi wa masuala ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi James Bwana akiongea na wadau kwenye mkutano wa kujadili masuala yaushirikishwaji wa Diaspora katika shughuli za kiuchumi nchini uliofanyika jijini Dodoma
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje naUshirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Agnes Kayola akifunguamkutano wa wadau kujadili masuala ya ushirikishwaji wa Diasporakatika shughuli za maendeleo nchini uliofanyika jijini Dodoma
Mkurugenzi wa masuala ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi James Bwana akifuatilia majadala uliokuwa ukiendelea kuhusu ushirikishwaji wa Diaspora katika shughuli za maendeleo nchini uliofanyika jijini Dodoma
Meza kuu; Mkurugenzi wa masuala ya Diaspora katika Wizaraya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki BaloziJames Bwana (kushoto) Kaimu Naibu Katibu Mkuu Balozi Agnes Kayola (katika) na Naibu Mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano waKimataifa na Diaspora, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Bi. Maryam Ramadhan Hamoud wakifuatilia mkutano
Sehemu ya wadau wakifuatilia mkutano wa kujadili masuala yaushirikishwaji wa Diaspora katika shughuli za maendeleo nchini uliofanyika jijini Dodoma
Sehemu ya wadau wakifuatilia mkutano wa kujadili masuala yaushirikishwaji wa Diaspora katika shughuli za maendeleo nchini uliofanyika jijini Dodoma
Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadauwalioshiriki mkutano wa kujadili masuala ya ushirikishwaji wa Diaspora katika shughuli za maendeleo nchini uliofanyika jijini Dodoma

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.