Friday, September 23, 2022

DKT MPANGO AHUTUBIA BARAZA. KUU LA UMOJA WA MATAIFA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Philip Mpango akihutubia Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan jijini New York nchini Marekani.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Philip Mpango akihutubia Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Philip Mpango akihutubia Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (kushoto) Waziri wa Nchi Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa Zanzibar Mhe. Masoud Ali Mohammed , Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu na Mama Dionisia Mpango Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais Dkt. Mpango katika Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijijini New York nchini Marekani 

 


 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inaamini diplomasia na meza za mazungumzo ni chombo bora cha kutatua migogoro duniani na kwamba nchi zina wajibu wa kuzingatia utatuzi wa migogoro kwa njia za amani ili kulinda ustawi wa watu watu na kuepuka athari zinazoweza tokana na migogoro duniani.

Mhe. Dkt. Mpango amesema hayo jijini New York alipohutubia Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) alipomuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

“Tanzania inaamini kuwa diplomasia na meza za mazungumzo ndiyo chombo muhimu na ni vitu vikuu vya kuzingatia wakati wa  kutatua migogoro duniani, Mataifa yanapaswa kuzingatia kuwa yanahaki na wajibu wa kulinda maisha ya binadamu hasa watoto na wanawake lakini pia lazima wahakikishe ustawi wa watu wote , ni muhimu  kutafuta suluhu au kutatua migogoro kwa njia za amani, hii inasaidia kuepuka athari zitokanazo na migogoro hiyo kama vile ongezeko la bei za chakula na mafuta na kushuka kwa uzalishaji wa kilimo na viwanda duniani kote,“ alisema Dkt. Mpango.

Makamu wa Rais pia amepongeza juhudi za Umoja wa Mataifa katika kukuza lugha mbalimbali duniani ikiwemo tamko la kihistoria la Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) lililoitaja "7 Julai" kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani na kuwezesha lugha hiyo kuadhimishwa kwa mara ya kwanza duniani na hivyo kuitambua arsmi kimataifa.

Amesema Tanzania inajivunia kushiriki katika shughuli za kulinda amani ambapo imechangia Askari katika misheni 5 kati ya 16 zilizopo za kulinda amani duniani na kuahidi kuwa  itaendelea kuchangia zaidi iwapo itaombwa kufanya hivyo na kuiomba Umoja wa Mataifa kuongeza uungaji mkono wake kwa juhudi za kikanda katika za kujenga na kulinda amani.

 

Kuhusu mabadiliko ya tabia nchi Dkt. Mpango amesema nchi za Afrika zinahitaji mabadiliko ya haki na utaratibu katika kufikia matumizi ya nishati mbadala kwa kuzingatia hali za Maisha ya watu wa bara hilo wenye changamoto mbalimbali za upatikanaji wa nishati hizo na kutoa wito wa kuondolewa kwa upinzani dhidi ya ufadhili wa kimataifa katika utekelezaji wa miradi ya mageuzi katika nchi za Afrika ambayo inalenga kutumia rasilimali ikiwemo gesi kwa ajili ya nishati na matumizi mengine katika kufikia maendeleo.

 

Amesema biashara ya hewa ukaa barani Afrika inapaswa kufanyika kwa uwazi na kuwanufaisha wananchi waliotunza mazingira na misitu inayozalisha hewa hiyo kwa matumizi ya dunia na kuongeza kuwa Tanzania ni moja ya iliyowekeza zaidi katika uhifadhi wa misitu ambapo asilimia 30 ya eneo la ardhi ya taifa hilo imehifadhiwa.

 Kuhusu mapambano ya ugonjwa wa COVID 19, Dkt. Mpango amesema amezishukuru nchi na jumuiya za kimataifa zilizoshirikiana na Tanzania kupambana na janga hilo kuanzia utoaji wa vifaa vya uchunguzi, dawa, programu za msaada wa chanjo, ambazo zimekuwa muhimu katika kushinda vita dhidi ya janga hilo na kuwezesha nchi kufikia asilimia 60 ya kuchanja watu wake hadi sasa na kuongeza kuwa kuchelewa kwa Afrika kupata chanjo za ugonjwa huo kunasisitza hitaji la Nchi za Kiafrika kufanya kazi pamoja katika ukuzaji wa masuluhisho asilia kupitia utafiti wa pamoja wa kisayansi.

Ametoa wito kwa mataifa kuweka vipaumbele vya vitendo hasa kwenye malengo ya maendeleo endelevu ambapo amayasihi mataifa kujitolea kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa na Nchi Wanachama wake, kwa nia ya ushirikiano na mshikamano wa kimataifa kuelekea mustakabali endelevu.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.