Thursday, September 8, 2022

RAIS SAMIA AIELEKEZANDC KUTOA KIPAOMBELE KWA WANAWAKE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama,Wizara na taasisi mbalimbali kuwateuwa washiriki wenye sifa hususan vijana na kuwapa kipaumbele wanawake kushiriki mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).

Mhe. Rais Samia ametoa maelekezo hayo Septemba 8, 2022 wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Taifa cha Ulinzi mwaka 2012.

Mhe. Samia alisema kuna umuhimu wa kuwapa kipaumbele wanawake ili waweze kupata mafunzo hali itakayosaidia kuongeza tija na ufanisi katika maeneo yao ya kazi na Taifa kwa ujumla kwani ukimuelimisha mwanamke umeelimisha jamii.

Alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana kwenye kipindi cha miaka kumi anapenda kuona masuala muhimu yanatimia katika muda mfupi ikiwemo kwenda kuwafundisha watu wa ngazi za chini kwenye Serikali za Mikoa na  Wilaya kwani huko ndio kuna kundi kubwa la watu.

"Mafunzo yanayotolewa kwenye ngazi za juu ni lazima yashuke chini ili wafundishwe na kupata uelewa wa masuala ya msingi ya usalama na kuitumikia nchi kizalendo.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax alisema kuwepo kwa chuo hicho nchini kimeliwezesha Jeshi la Tanzania kutoa mafunzo kwa maafisa wakuu wengi zaidi tofauti na awali ambapo Jeshi lililazimika kuwapeleka maafisa wake kupata mafunzo hayo nje ya nchi.

Aliongeza kuwa NDC imewezesha kutoa mafunzo kwa idara nyingine za Serikali na viongozi mbalimbali kwa kuwajengea uelewa wa pamoja juu ya usalama.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni mdau muhimu kwa maendeleo ya Chuo Cha Taifa Cha Ulinzi ambapo hadi sasa Wizara imeendelea kupeleka washiriki kwenye kozi ndefu na fupi ambapo miongoni mwao Wanawake wawili walioshiriki kozi ndefu walitunikiwa tuzo za uongozi kwa nyakati tofauti.

Wanawake hao ni Mkurugenzi wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, Balozi Mindi Kasiga mwaka 2019 pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Itifaki, Bi. Naomi Zegezege mwaka 2022 wote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kadhalika, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika mahojiano binafsi alisema kuwa Chuo Cha NDC kimekuwa msaada mkubwa katika kuwanoa viongozi mbalimbali na baadhi ya watumishi wizarani kujengewa uwezo jambo ambalo limeongeza ufanisi kazini.

"Kila mwaka tumekuwa tukipeleka watumishi wawili katika Mafunzo ya muda mrefu NDC na matunda ya mafunzo hayo yamekuwa chanya kwa Wizara ninayoisimamia, natumaini kuwa tutaendelea kuwapeleka watumishi wengi zaidi baadae hususan Wanawake ili kuwajengea uwezo zaidi wa kujiamini wakati wanapotekeleza majukumu Yao," alisema Balozi Mulamula
Hafla ya Maadhimisho ya miaka 10 ya NDC ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Taifa cha Ulinzi mwaka 2012 
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambio ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Midni Kasiga (wa kwanza kushoto) akiwa na baadhi ya viongozi waliopata fursa ya kusoma kozi za muda mrefu  katika Chuo cha NDC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) (katikati) pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Mchemba (Mb.) wakizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa (Mb.) waliposhiriki katika hafla ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Taifa cha Ulinzi mwaka 2012

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiteta jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa (Mb.) wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Taifa cha Ulinzi mwaka 2012

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika picha ya pamoja na Viongozi waandamizi wa Serikali na Wahitimu wa NDC

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.