Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman amesema Serikali ya Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwawezesha Wawekezaji wenye tija kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Uchumi wa Bluu.
Mhe. Othman ametoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi Kongamano la Pili la
Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Zanzibar tarehe
28 Septemba, 2022 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya biashara na
uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.
Mhe. Othman ambaye alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye kongamano hilo amesema Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imefungua milango kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali na kwamba inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara
kwa kuzifanyia maboresho sheria na kanuni mbalimbali za uwekezaji.
Kadhalika alisema maboresho hayo yanakwenda sambamba na yale ya sekta ya utoaji huduma kama vile za viza, vibali vya kazi na ukaazi pamoja na kuboresha mawasiliano kupitia mifumo ya kidigitali ambapo Serikali hiyo inatarajia hivi karibuni kuzindua mfumo wa uombaji viza kwa njia ya mtandao.
"Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya
uwekezaji ili kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa
maeneo bora ya uwekezaji duniani. Uwekezaji una manufaa
makubwa ya kiuchumi kwa nchi ikiwa ni pamoja na kukuza pato la taifa pamoja na kutenegeneza ajira kwa vijana na wanawake
" alisema Mhe. Othman.
Mhe. Othman ameeleza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi
Novemba 2020 hadi wakati wa kongamano hilo Zanzibar imesajili miradi ya uwekezaji
196 yenye thamani ya dola za marekani bilioni 1. 4 ambapo miradi hiyo inatarajiwa
kutengeneza ajira zipatazo 9,000. Hivyo alihimiza
washiriki kutumia Kongamano hilo kama chachu ya kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi
kuja nchini.
“Kongamano hili liwe chachu ya kuvutia na kuhamasisha wawekezaji zaidi kuja Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Naendelea kutoa wito kwa wawekezaji kutoka Italia na duniani kote kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji tulizonazo. Namaliza kwa kusema Wekeza Zanzibar, Wekeza sasa” alisisitiza Mhe. Othman
Awali akizungumza wakati wa kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga amepongeza jitihada zinazofanywa
na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Balozi
mwenzake wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi za kuandaa kongamano hilo
kwa mara ya pili ikiwa ni mchango wao wa kuhakikisha nchi hizi mbili zinanufaika
kupitia ushirikiano mzuri uliopo.
Pia aliwataka washiriki wote kutumia kongamano hilo kama fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu miongoni mwao ili kuendelea kuboresha sekta ya biashara na uwekezaji nchini.
Mhe. Soraga pia alitumia fursa hiyo kuainisha fursa za
kipaumbele za uwekezaji Zanzibar kuwa ni pamoja na Sekta ya Uchumi wa Bluu, Kilimo, Usindikaji wa mazao ya kilimo, Utalii, ufugaji wa samaki, utalii unaozingatia
utunzaji wa mazingira , miundombinu, nishati na uwekezaji katika mali
zisizohamishika kama majengo.
Wakati wa Kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo Maendeleo ya Miundombinu, Uchumi wa Bluu na Kilimobiashara na Kilimo cha Kisasa cha kutumia mashine na mitambo. Kongamano hilo ambalo limewashrikisha wadau kutoka sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji wa hapa nchini na kutoka Italia litahitimishwa rasmi tarehe 30 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Washiriki wa Kongamano wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman |
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga nae akizungumza wakati wa Kongamano hilo |
Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mhe Soraga |
Mkurugezni Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) akifafanunua fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Zanzibar |
Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (kushoto) na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (katikati) |
Sehemu ya washiriki wa kongamano |
Sehemu nyingine ya washiriki |
Mhe. Balozi Lombardi akizungumza na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar, Bi. Leluu Abdallah (kushoto) na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Salma Baraka |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.