Tuesday, September 20, 2022

DKT. MPANGO : TUJITOE UPYA NA KUONGEZA UWEKEZAJI KATIKA ELIMU

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mageuzi katika sekta ya elimu ulioshirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, Wakuu wa Taasisi na Mashirika na wadau wa elimu jijini New York , Marekani tarehe 19 Septemba, 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa waliposhiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mageuzi katika sekta ya elimu ulioshirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, Wakuu wa Taasisi na Mashirika na wadau wa elimu jijini New York , Marekani tarehe 19 Septemba, 2022

 


 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema  Mataifa yanapaswa kujitoa upya na kuongeza uwekezaji  zaidi katika sekta ya elimu ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na ya uhakika katika kuelekea mwaka 2030.

 

Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema hayo alipohutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliobeba ajenda ya Mageuzi katika sekta ya elimu ulioshirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, Wakuu wa Taasisi na Mashirika na wadau wa elimu jijini New York , Marekani tarehe 19 Septemba, 2022

Makamu wa Rais amesema elimu ni sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo 2030 hivyo hakuna budi kuchukua hatua katika kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo na kuongeza kuwa kupatikana kwa elimu bora kutapunguza matabaka katika ajira pamoja na kipato baina ya wananchi.

 

Amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha sekta ya elimu ikiwemo kuanza mchakato wa kuboresha mitaala kwa kuwashirikisha wadau wa elimu, kuwekeza katika vyuo vya ufundi stadi na mafunzo , kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuongeza bajeti ya wizara husika kufikia asilimia 18 ya bajeti yote ya serikali.

 

Amesema Serikali ya Tanzania inahakikisha upatikanaji wa elimu jumuishi kwa wote bila kujali jinsia , ulemavu na hali ya uchumi na kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia Serikali  pia imedhamiria kuboresha usimamizi wa nguvu kazi ya walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji bora kwa kuwajengea uwezo walimu na maofisa elimu kuhusu uunganishaji wa teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji  na uandaaji  wa masomo ya kidijitali.

 

Makamu wa Rais Dkt. Mpango, yupo nchini Marekani kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.