Saturday, October 29, 2022

TANZANIA, MALAWI KUSHIRIKIANA KATIKA MUSUALA YA ULINZI NA USALAMA

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi zimesaini hati mbili za makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (The 5th Joint-Permanent Commission for Cooperation - JPCC) kati ya nchi hizo mbili uliofikia tamati jana tarehe 28 Oktoba 2022 jijini Dar es Salaam.

Hati hizo za makubaliano zilizosainiwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) na Mhe. Titus Mvalo Waziri wa Sheria wa nchini Malawi zinahusu ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi la Malawi na Jeshi la Polisi la Tanzania, na ushirikiano baina ya Taasisi za Uhamiaji za pande zote mbili. 

Akizungumza muda mfupi baada ya kusaini hati hizo, Waziri Ndumbaro na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo, ambaye pia alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ameeleza kuwa Mkutano huo umewezesha pande hizo mbili kukubaliana katika masuala mbalimbali ya msingi huku msisitizo mkubwa ukielekezwa katika sekta ya Biashara, Uwekezaji, Ulinzi na Usalama, Miundombinu, Masuala ya Mambo ya Nje na Kijamii 

“Katika Mkutano huu wa Tano wa JPCC pamoja na masuala mengine nchi zetu mbili zimekubaliana kuongeza kasi ya kutatua changamoto zinazokabili sekta binafsi ili kuwezesha na kurahisisha biashara, vilevile tumekubalia kutumia fursa ya uwepo wa Ziwa Nyasa katika kurahisisha uendeshaji wa shuguli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji wa bidhaa, huduma na watu kwa maendeleo ya wananchi wetu” alisema Dkt. Ndumbaro.

Waziri Mdumbaro aliongeza kutaja fursa na faida mbalimbali zilizotokana na Mkutano huo ikiwemo, nia na dhamira ya Nchi ya Malawi ya kutumia barabara ya Mtwara hadi Bandari Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma katika kusafirisha bidhaa na huduma kwenda nchini humo. Fursa nyingine ni nia ya Malawi kushirikiana na Tanzania katika suala la elimu na mfunzo kupitia Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaa, ambapo alieleza kuwa hati ya makubaliano kuhusiana na suala hilo inatarajiwa kusainiwa siku za usoni. 

Dkt. Ndumbaro aliendelea kufanunua kuwa licha ushirikiano na uhusiano mzuri wa Kidiplomasia uliopo baina ya pande hizo mbili, Malawi imeonesha nia ya kutumia Bandari ya Mtwara na Mbamba Bay kutokana na ukweli kuwa njia hiyo ni fupi zaidi ikilinganishwa na njia zote wanazozitumia hivi sasa kutoka Bandari mbalimbali kuingiza bidhaa nchini humo. 

Mbali na kuzungumzia fursa za kiuchumi Dkt. Ndumbaro, alitoa rai kwa Serikali ya Jamhuri ya Malawi kuendelea kuthamini lugha ya Kiswahili sambamba na kuhimiza matumizi ya lugha hiyo nchini humo. Vilevile aligusia umuhimu wa Serikali ya Jamhuri ya Malawi kuendelea kufundisha somo la Kiswahili katika ngazi mbalimbali za elimu nchini humo.

Kwa upande wake Mhe. Titus Mvalo, Waziri wa Sheria wa Malawi na Kiongozi wa Ujumbe wa Malawi ambaye pia alikuwa anamwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo amebainisha kuwa, masuala yote katika Mkutano huo yamehafikiwa katika wakati sahihi ambapo Viongozi Wakuu wa Serikali za pande zote mbili wanania ya dhati kuona ushirikiano wa Tanzania na Malawi unaleta tija ya kiuchumi kwa wananchi wa pande zote mbili. 

Waziri Mvalo aliendelea kuelezea namna Serikali ya Malawi inaweka jitihada katika kukuza lugha ya Kiswahili nchini humo ikiwemo kuongeza somo la kiswahili kwenye mtaala wa elimu nchini humo.

“Moja ya sifa kubwa ya lugha ya Kiswahili ni ile ya kutokuwa na mizizi ya ukabila, siyo rahisi hata hapa nchini Tanzania kusikia kabila moja wapo miongoni mwa makabila zaidi ya 120 yaliyopo likijinasibu kuwa lugha ya kiswahili ya kwake. Tunajivunia lugha hii hadhimu ya Kiswahili kwa kuwa ni lugha ya asili ya Afrika inayounganisha watu wengi barani hapa” alisema Waziri Mvalo 

Akihitimisha hotuba yake ya kufunga Mkutano wa Tano wa JPCC Waziri Mvalo ametoa rai kwa sekta zote kuhakisha wanakutana mara kwa mara ili kufuatilia utekelezaji wa masuala yote yaliyohafikiwa katika Mkutano huo. 

Mkutano wa Tano wa JPCC ambao umehitimishwa katika ngazi ya Mawaziri umefanyika kwa kipindi cha siku tatu kuanzia terehe 26 - 28 Oktoba 2022. Mbali na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro kwa upande wa Tanzania Mkutano pia ulihudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa. Wengine waliohudhuria ni Watendaji kutoka Wizara, Idara, na Taasisi mbalimbali za Serikali. 
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akisalimiana na Waziri wa Sheria wa nchini Malawi Mhe. Titus Mvalo kwenye wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa (kulia) akifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akifungua Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Sheria wa nchini Malawi Mhe. Titus Mvalo akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Waziri wa Sheria wa nchini Malawi Mhe. Titus Mvalo wakibadilishana nyaraka kwenye Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Waziri wa Sheria wa nchini Malawi Mhe. Titus Mvalo wakisaini Hati za Makubaliano kwenye Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Azizi akitoa neno la ukaribisho wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Humphrey Polepole akifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea
Sehemu ya Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam
Picha ya pamoja
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally S. Gugu na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Bw. Kheri Abdul Mahimbali wakibadilishana mawazo wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam
Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi ukiendelea

Thursday, October 27, 2022

DIASPORA WAHIMIZWA KUTUMIA HUDUMA ZA FEDHA ZA KIDIGITALI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewasisitiza Diaspora wote Duniani kutumia huduma za kifedha kupitia kwa watoa huduma waliosajiliwa ili kuendelea kuchangia uchumi wa Tanzania.

Dkt. Tax ametoa wito huo jijini Dar es Salaam aliposhiriki uzinduzi wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyoanzishwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kupitia huduma ya kutuma fedha ya M-Pesa.

Amesema, upo umuhimu mkubwa kwa Diaspora kutumia huduma za kifedha zilizosajiliwa ili kuhakikisha usalama wa fedha zao na kuweka kumbukumbu sawa. Amesema kwa mujubu wa Takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania Diaspora walichangia uchumi wa Taifa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 30 mwaka 2019 na mwaka 2021 Diaspora walichangia uchumi wa Taifa kwa Dola za Kimarekani milioni 569 sawa na kuchangia asilimia 0.8 ya pato la Taifa.

Mhe. Dkt. Tax ameipongeza Kampuni ya Vodacom kwa kuwekeza katika ubunifu na kuboresha huduma zao wakati wote ili kuendana na mahitaji ya wananchi kulingana na mabadiliko ya Teknolojia. 

Amesema anaipongeza Kampuni hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiunganisha Afrika kupitia huduma zao ambapo kwa sasa wamepanua wigo kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kuongeza ukanda wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) jambo ambalo litawawezesha Diaspora kwenye maeneo hayo kutuma na kupokea fedha pasipo kikwazo chochote.

“Sekta ya fedha ni sekta muhimu katika nchi yoyote, Serikali inaona jambo hili ni kubwa kwa sababu ya umuhimu wa sekta ya fedha lakini kwa kutambua kwa sasa dunia ipo katika uchumi wa kidigitali. Uchumi wa kidigitali unafanya kazi kidigitali hivyo nawasihi Diaspora kutumia huduma hii ili kuweza kuchangia maendeleo ya taifa kwa kuwa benki na taasisi nyingine zinazotoa huduma za kifedha zimerahisisha biashara na uwekezaji na shughuli za kiuchumi kwa ujumla,” alisema Dkt. Tax.

Kadhalika Mhe. Dkt. Tax ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kutoa miongozo mbalimbali inayowawezesha watoa huduma za fedha nchini kuandaa huduma zenye manufaa kwa wanannchi na kuahidi Serikali kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi ili kutimiza lengo la kuwainua wananchi kiuchumi kupitia huduma mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Vodacom M-pesa, Bw. Epimack Mbeteni amesema kuzinduliwa kwa huduma ya M-Pesa katika ukanda wa SADC kumetoa fursa ya kuongeza wigo wa kutuma na kupokea pesa katika nchi nyingi zaidi barani Afrika hususan nchi za SADC.  

“Wateja wetu wanaweza kupokea na kutuma fedha katika ukanda wa Sadc, sasa tumeiunganisha Afrika na M-Pesa, jambo hili litachangia ukuaji wa uchumi wa taifa letu,” amesema Bw. Mbeteni

Bw. Mbeteni ameongeza kuwa uzinduzi wa huduma hiyo utarahisisha ufanyaji wa biashara na huduma nyingine za kijamii. Uzinduzi wa huduma hiyo uliongozwa na kauli mbiu ya “Dunia Kijiji, Afrika ni M-Pesa”.  Katika uzinduzi huo, Dkt. Tax aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Godwin Gondwe.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwasilisha hotuba ya ufunguzi aliposhiriki uzinduzi wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyoanzishwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kupitia huduma ya kutuma fedha ya M-Pesa  

Mkurugenzi wa Vodacom M-pesa, Bw. Epimack Mbeteni akiongea na washiriki wakati wa uzinduzi wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)

Washiriki wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za SADC

Washiriki wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Godwin Gondwe na wafanyakazi wa Kampuni ya simu ya Vodacom



Wednesday, October 26, 2022

TANZANA-MALAWI WAKUTANA KUJADILI MASUALA YA USHIRIKIANO


Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (The 5th Joint-Permanent Commission For Cooperation - JPCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi umeanza leo tarehe 26 Oktoba 2022 jijini Dar es Salam. 

Mkutano huu wa siku tatu, kuanzia tarehe 26 – 28 Oktoba 2022, utafanyika katika ngazi ya Wataalamu Waandamizi tarehe 26 Oktoba 2022, Makatibu Wakuu tarehe 27 Oktoba 2022, na kuhitimishwa na Mawaziri tarehe 28 Oktoba 2022. 

Agenda za mkutano huu zinaangazia masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, kilimo, afya, ulinzi na usalama, usafirishaji, sekta ya mafuta, maliasili, masuala ya utafiti na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Vilevile Mkutano huu utajadili namna ya kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vya forodha ili kurahisisha ufanyaji wa biashara baina ya mataifa haya mawili. 

Akifungua Mkutano huo katika ngazi ya Wataalamu Waandamizi, Balozi Joseph Sokoine Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ameeleza mkutano huo ni kielelezo tosha kuwa Serikali za pande zote mbili zinaendelea kutambua na kuthamini umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na karibu zaidi ili kuchochea maendeleo ya shughuli mbalimbali za kijamii na uchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Aidha Balozi Sokoine ametoa rai kwa wataalamu waandamizi wa pande zote mbili kuhakikisha kuwa wanatumia mkutano huo kujadili na kuweka mikakati madhubuti ili kutengeneza mazingira wezeshi kwa mataifa hayo mawili yenye utajiri wa fursa na rasilimali, kuweza kuchochea kasi ya maendeleo siyo tu kwa faida ya mataifa hayo mawili bali kwa faida ya kikanda na kimataifa kwa ujumla

“Sote tunatambua kuwa mataifa yetu yameendelea kufarahia ushirikiano mzuri uliopo baina yetu ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na mifumo mizuri ya kisheria inayotuwezesha kukutana na kujadili masuala yanayotuhusu mara kwa mara. Natoa rai kwenu kutumia mkutano huu vyema katika kujadili kwa kina kuhusu masuala muhimu kwa maslahi na maendeleo ya pande zote mbili” alisema Balozi Sokoine. 

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikiongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiendelea kuendesha programu na kuchukua hatua mbalimbali katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi sambamba na kudumisha Uhusiano wa Kidiplomasia na Mataifa mbalimba duniani. 

Kwa upande wa Malawi, Ubalozi wa Tanzania nchini humo chini ya Mhe. Balozi Humphrey Polepole sambamba na kuendelea dumisha Uhusiano wa Kidiplomasia umekuwa ukiendelea na utekelezaji wa mikakati inayoliwezesha Taifa kunufaika na fursa za kiuchumi zinazopatikana nchini humo. 

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), biashara kati ya Tanzania na Malawi imeendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 138.12 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 186.1 mwaka 2019. Kutokana na janga la UVIKO-19 mwaka 2020, biashara ilipungua na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 159.4. Hata hivyo mwaka 2021 biashara iliongezeka tena hadi kufikia shilingi milioni 198.3.

Ujumbe wa Malawi katika Mkutano huo umeongozwa na Bw. William Kantayeni ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchini humo. 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofayika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Azizi akichangia jambo kwenye Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.

Picha ya pamoja

Sehemu ya ujumbe wa Malawi wakifuatilia Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Malawi Bw. William Kantayeni akichangia jambo kwenye Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Balozi Humphrey Polepole akifuatilia mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.

Meza kuu wakifuatilia Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea katika ukumbi wa Mikutano wa Kamataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam

DKT. TAX APOKEA UJUMBE MAALUM KUTOKA MISRI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Hassan Shoukry uliowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika wa nchi hiyo, Mhe. Sherif Issa.

 

Akizungumza mara baada ya kupokea ujumbe huo leo tarehe 26 Oktoba 2022 jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Tax ameishukuru Serikali ya Misri kwa kuendelea kuthamini ushirikiano wa kihistoria uliopo baina yake na Tanzania hususan kwenye sekta ambazo zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja kama afya, elimu, maji, nishati na ujenzi wa miundombinu.

 

Amesema, ni kutokana na kuthamini mchango unaotolewa na Misri kwenye sekta mbalimbali za maendeleo nchini Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara nchini humo mwezi  Novemba 2021 na maeneo mbalimbali ya ushirikiano yalijadiliwa na kukubalika.

 

“Ninayo furaha kukukaribisha nchini Mhe. Waziri. Nakiri kupokea ujumbe huu muhimu kutoka kwa Waziri mwenzangu. Nitaupitia na kuufanyia kazi na kuwasilisha kwenu mrejesho haraka iwezekanavyo”, amesema Mhe. Dkt. Tax.

 

Naye, Mhe. Issa amempongeza Mhe. Dkt. Tax kwa kuteuliwa katika wadhifa huo mpya na kumweleza utayari wa Serikali ya Misri katika kushirikiana naye.

 

Kadhalika amesema,  Serikali ya Misri itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutekeleza na kukamilisha miradi yote ya pamoja ambayo nchi hizo zimekubaliana ukiwemo Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere.

 

“Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere ni  kwa ajili ya Watanzania. Mradi huu ni mkubwa na wa kwanza kwa Misri kuutekekeleza hapa nchini. Hivyo tutajitahidi kama Serikali kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha mradi wote unakamilika na kukabidhiwa”, alisisitiza Mhe. Issa.

 

Pia  Mhe. Issa alitumia nafasi hiyo kuikaribisha Tanzania kushirki kwenye Mkutano wa 27 wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika mwezi Novemba 2022 katika Mji wa Sharm El Sheikh, nchini humo.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ambaye alishiriki mazungumzo hayo amesema, Mradi  wa Bwawa la Kufua Umeme wa Julius Nyerere ni alama ya ushirkiano kati ya Tanzania na Misri na kwamba Wizara yake itaendelea  kutoa ushirikiano wote unaohitajika kwa Serikali ya Misri na Timu ya Wataalam wa Mradi huo ili kuufanikisha.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea ujumbe maalum kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Hassan Shoukry uliowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia masuala ya Afrika wa nchi hiyo, Mhe. Sherif Issa.Mhe. Dkt. Tax amepokea ujumbe huo leo tarehe 26 Oktoba, 2022 akiwa katika Ofisi Ndogo za Wizara zilizopo jijini Dar es Salaam

Mhe. Dkt. Tax akiwa katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia masuala ya Afrika,  Mhe. Sherif Issa  
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ambaye alishiriki mazungumzo hayo naye akichangia jambo
Mazungumzo yakiendelea

Mhe. Dkt. Tax na mgeni wake wakimsikiliza Balozi wa Misri hapa nchini Mhe. Mohammed Gaber Abulwafa wakati akifafanua jambo

 Mhe. Makamba akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Maharage Chande pamoja na wadau wengine wakaishiriki mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Issa (hawapo pichani)

Picha ya pamoja

UMOJA WA ULAYA KUIPATIA TANZANIA MSAADA WA EURO MILIONI 166



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kulia) akiwa na Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen kabla ya kuanza mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen. Kushoto kwa Mhe. Waziri ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na katika Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Nyamanga. 

Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen (katikati) na ujumbe wake wakisikiliza jambo kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam

Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na katika Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Nyamanga akisalimiana na .Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen alipowasili kwenye ofisi za Wizara kwa ajili ya mazungumzo 
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akisalimiana na Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen alipowasili kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere kwa ajili ya kufanya mazungumzo

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen yaliyofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere






 

Tuesday, October 25, 2022

DKT. MWINYI AWATAKA MABALOZI KUZINGATIA MASLAHI YA TAIFA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka Mabalozi wa Tanzania Nje ya nchi kuzingatia maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanapotekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi.

Dkt. Mwinyi ametoa agizo hilo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipofika Ikulu, Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022 kwa ajili ya kujitambulisha. 

“Mabalozi wa Tanzania Nje ya nchi wahakikishe wanaangalia maslahi mapana ya Tanzania wanapotekeleza diplomasia ya uchumi, hususan uchumi wa buluu ambao ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” amesema Dkt. Mwinyi

Kwa Upande wake, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameahidi kuyafanyia kazi maagizo na miongozo mbalimbali inayotolewa na itakayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa weledi na wakati.

“Mhe. Rais napenda kukuhakikishia kuwa nitasimamia na kutekeleza yote uliyotuelekeza kwa wakati na kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” amesema Dkt. Tax

Katika ziara hiyo, Dkt. Tax alipata fursa pia ya kujitambulisha kwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla. 

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wameahidi kumpatia ushirikiano unaohitajika ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.

Naye Dkt. Tax amesema yupo tayari kwa ajili ya kazi ya kuitumikia nchi na kuhakikisha ushirikishwaji wa Zanzibar juu ya mambo ya muungano sambamba na fursa mbalimbali ikiwemo maazimio yanayopitishwa mbele ya jumuiya za kikanda na za kimataifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipofika Ikulu, Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipofika Ikulu, Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa Ofisini kwake Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa Ofisini kwake Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa Ofisini kwake Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimueleza jambo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla. Dkt. Tax alifika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais kwa lengo la kujitambulisha 



KATIBU MTENDAJI WA SADC AFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI

Tanzania itaendelea kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)ili kufikia malengo ya kukuza uchumi na kudumisha amani na usalama katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.



Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokutana kwa mazungumzo na Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Mpedi Magosi wakati wa ziara yake ya kikazi nchini hivi karibuni.



Mhe. Dkt. Tax amesema lengo kuu la Jumuiya hiyo ni kuziwezesha kujikomboa kiuchumi nchi za Kusini mwa Afrika. Lakini pia kuhakikisha nchi za ukanda huo zinakuwa na amani na utulivu, hivyo Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi zozote zinazofanywa na Sekretarieti hiyo ili kufikia malengo hayo.



Pia alivitaja vipaumbele vya Tanzania kwenye Jumuiya hiyo kuwa ni pamoja na Amani na Usalama, Kilimo, Uchumi wa Buluu, maendeleo ya Miundombinu na uchumi  wa kidigitali.



Ameongeza kusema kazi kubwa ya Sekretarieti hiyo ni kusimamia kwa bidii utekelezaji wa mipango, itifaki, na mikataba mbalimbali iliyokwishapitishwa au kuridhiwa na nchi wanachama.


"Nakushukuru sana kwa kutenga muda wako na kuja kutembelea Tanzania. Nakupongeza pia kwa kazi nzuri unayoendelea kufanya ya kuongoza chombo muhimu kinachosimia utekelezaji wa malengo ya Jumuiya yetu. Ushauri wangu kwako ni kuendelea kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali ambayo tayari yapo kwa ajili ya utekelezaji" alisema Mhe. Dkt. Tax.



Kadhalika alimkumbusha Mhe. Magosi kuendeleza jitihada za kutangaza majukumu na umuhimu wa Jumuiya hiyo katika Nchi Wanachama kwani bado Agenda na Madhumuni ya Jumuiya hayajulikani ipasavyo miongoni mwa wananchi katika Nchi Wanachama.

 

Kwa upande  wake, Mhe. Magosi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Dkt. Tax kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo mpya na kumuahidi ushirikiano wake binafsi na kutoka katika Sekretarieti. Pia alimpongeza kwa uongozi makini wa miaka nane kama Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC  hususan katika uandaaji wa nyaraka ikiwemo  Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC wa mwaka 2020-2030.



Pia aliipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ugaidi na kwamba uwepo wa kituo hicho hapa nchini kunadhihirisha utayari wa Tanzania katika kuhakikisha suala la usalama katika kanda linapewa kipaumbele.



Wakati wa ziara hiyo ya siku mbili hapa nchini kuanzia tarehe 24 hadi 25 Oktoba, 2022, Mhe. Magosi amekutana kwa mazungumzo na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametembelea Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ugaidi pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD). 

 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Mhe. Elias Masego alipomtembelea jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Mhe. Masego yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 24 hadi 25 Oktoba 2022.
Mhe. Masego akizungumza wakati wa kikao kati yake na Mhe. Dkt. Tax
Ujumbe uliofuatana na Mhe. Masego wakifutilia kikao

Ujumbe wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola (kushoto) wakifuatilia mazungumzo
Mhe. Masego akimpatia zawadi Mhe. Dkt. Tax

Picha ya pamoja
Mhe. Masego akizunguza wakati alipotembelea Kituo cha Kikanda cha SADC cha Kupambana na Ugaidi kilichopo Dar es Salaam

Mhe. Masego alipotembelea Kituo cha Kikanda cha SADC cha Kupambana na Ugaidi 
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Kayola (kushoto) wakati wa ziara ya Mhe. Masego kwenye Kituo cha Kupambana na Ugaidi 
Kikao kikiendelea
Kaimu Mkurugenzi wa Bahari Kuu ya Dawa (MSD), Bw. Leopold Shayo akizungumza wakati wa ziara ya Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Masego kwenye Bohari hiyo. Kushoto ni Mhe. Masego akimsikiliza. Mhe. Masego ametembelea Bohari hiyo kutokana na kushinda zabuni ya kusambaza dawa na vifaa tiba kwa nchi za SADC
Kikao kati ya Mhe. Masego na MSD kikiendelea
Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Bw. Shayo akimsikiliza Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Masego (hayupo pichani)
Mhe. Masego akizungumza alipotembelea MSD
Mazungumzo yakiendelea

Mhe. Maseko akipokea zawadi ya barakoa zinazotengenezwa na MSD kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Bw. Shayo. 
Picha ya pamoja