Monday, October 10, 2022

TANZANIA KENYA ZAKUBALIANA KUENDELEA KUIMARISHA UHUSIANO

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yake na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yake na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto akimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipozungumza katika Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yao Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto akizungumza katika  Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yake na Mhe. Rais Samia Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto akizungumza katika  Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yake na Mhe. Rais Samia Ikulu jijini Dar es Salaam.



Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax kabla ya kuanza kwa Mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya Mhe. Dkt William Ruto baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.



Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Camilius Wambura akifuatilia Mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya Mhe. Dkt William Ruto baada ya kumalizika kwa  mazungumzo kati yao Ikulu jijini Dar es Salaam.


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman (kulia) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine wakifuatilia Mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya Mhe. Dkt William Ruto Ikulu jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga akifuatilia Mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya Mhe. Dkt William Ruto Ikulu jijini Dar es Salaam.


 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kenya zimekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi zao kwa manufaa ya pande zote mbili.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema hayo Ikulu jijini Dar wa Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea walichojadili katika mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto aliyekuwa na ziara ya kikazi ya siku mbili  nchini .

 

Ziara hii ya Mhe. Ruto nchini, imetuwezesha kujadili na kuhuisha mahusiano yetu na kutupa nafasi ya kujitathmini mashirikiano baina ya Tanzania na Kenya, na tumekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano baina yan chi zetu, alisema Mhe. Rais

 

Amesema katika mazungumzo yao wamejadili masuala ya kimkakati kuhusiana na ushirikiano baina ya nchi hizo, kikanda na kimataifa na kuongeza kuwa wamekubaliana kukuza na kuimarisha uhusiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Kenya.

 

Mhe. Rais Samia amesema Tanzania inajivunia kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya kodi ambavyo vilikuwa vinazuia ufanyaji wa Biashara kati ya Tanzania na Kenya.

 

“Wakati naingia madarakani kulikuwa na vikwazo visivyo vya kodi 68, lakini sasa vimefanyiwa kazi na kubaki 14, ni matarajio yetu kuwa vikwazo vilivyobaki navyo vitamalizwa na hivyo kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi zetu”, alisema Mhe. Rais.

 

Amesema wamekubaliana kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa Kenya kupitia Nairobi.

Amesema kuwa wamejadili jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa lengo la kuzifanya nchi zao kuwa sehemu salama  na kuongeza kuwa wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala ya kikanda na kimataifa na kukuza Jumuiya ya Afrika Mashariki Kama viongozi waanzilishi wa Jumuiya hiyo pamoja na nchi ya Uganda

 

Akizungumza katika mkutano huo Rais wa Kenya Mhe. William Ruto amesema amedhamiria kuyafikisha mahusiano kati ya Tanzania na Kenya katika levo nyingine na dhamira hiyo itafanikiwa kutokana na utayari uliopo baina ya nchi hizo.

 

Amesema biashara kati ya Tanzania imekuwa ikiongezeka na viongozi hao wanadhamira ya kuongeza ufanyaji wa biashara baina ya Kenya na Tanzania na kufafanua kuwa biashara kati ya nchi hizo  imeongezeka na kuifanya Tanzania kuwa mnufaika mkubwa kuliko ilivyokuwa awali.

 

“Mauzo ya Tanzania nchini Kenya yamekuwa yakiongezeka kwa kasi , kabla ya kuondolewa vikwazo visivyo vya kodi, sasa Kenya wananunua zaidi Tanzania kuliko ilivyo kuwa,” alisema

 

Amesema mauzo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 31 hadi shilingi bilioni 41 na biashara imekuwa kutoka shilingi bilioni 27 hadi shilingi bilioni 51 na hivyo kuleta picha kuwa Tanzania sasa inanufaika sana na ufanyaji wa biashara na Kenya.

 

Amesema wamekubaliana kuwa Mawaziri na wadau wengine wote wanaohusika na biashara wananakutana na kuzifanyia kazi changamoto zinazokabili sekta ya biashara baina ya nchi hizo ili wananchi waweze kufanya biashara .

 

Amesema uongozi wake utatilia mkazo na kuhakikisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es salaam hadi Mombasa unaharakishwa na kukamilika kwa wakati.

 

“Tutahakikisha tunatumia fursa ya ujenzi wa bomba la gesi kwenda Mombasa ili kuhakikisha tunatumia maliasili zetu na kuongeza ufanisi wa biashara na kuboresha maisha ya watu wetu, kuongeza na kuimarisha ushindani wa viwanda na wawekezaji wetu ,nchi zetu na ukanda wetu kwa ujumla

 

Amesema kukamilika kwa bomba hilo kutasaidia kukuza mpango wa viwanda katika nchi hizo na kuongeza kuwa utekelezaji wa mpango wa kuwa na mtandao mmoja kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki kwani walishakubaliana na baadhi ya nchi kuwa na mtandao mmoja

 

“Tutahakikisha tunatekeleza mpango huo ili kuwafanya wananchi wetu waweze kufanya biashara na kuwasiliana kwa urahisi na kwa gharama nafuu na hivyo kuendelea kuimarisha mahusiano yetu,” alsiema

 

Amesema wamewaelekeza watendaji katika nchi zao kukutana na kuandaa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya kabla mwaka huu haujaisha ili kujadili namna ya kuendelea kutatua changamoto zilizopo na hivyo kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo

 

Amewaambia Watanzania wajue kuwa wana marafiki na ndugu kutoka Kenya na kuahidi kuwa watafanya kazi pamoja na kuongeza kuwa Tanzania na Kenya hawawezi gawana njaa bali watagawana utajiri na fursa ili kujenga umoja kwa manufaa ya nchi zote mbili na watu wake

 

Rais Ruto aliwasili nchini tarehe 09/10/2022  kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili na aliondoka nchini kurejea Kenya tarehe 10/10/2022


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.