Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka Mabalozi wa Tanzania Nje ya nchi kuzingatia maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanapotekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi.
Dkt. Mwinyi ametoa agizo hilo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipofika Ikulu, Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022 kwa ajili ya kujitambulisha.
“Mabalozi wa Tanzania Nje ya nchi wahakikishe wanaangalia maslahi mapana ya Tanzania wanapotekeleza diplomasia ya uchumi, hususan uchumi wa buluu ambao ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” amesema Dkt. Mwinyi
Kwa Upande wake, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameahidi kuyafanyia kazi maagizo na miongozo mbalimbali inayotolewa na itakayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa weledi na wakati.
“Mhe. Rais napenda kukuhakikishia kuwa nitasimamia na kutekeleza yote uliyotuelekeza kwa wakati na kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” amesema Dkt. Tax
Katika ziara hiyo, Dkt. Tax alipata fursa pia ya kujitambulisha kwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wameahidi kumpatia ushirikiano unaohitajika ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.
Naye Dkt. Tax amesema yupo tayari kwa ajili ya kazi ya kuitumikia nchi na kuhakikisha ushirikishwaji wa Zanzibar juu ya mambo ya muungano sambamba na fursa mbalimbali ikiwemo maazimio yanayopitishwa mbele ya jumuiya za kikanda na za kimataifa.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.