Wednesday, October 12, 2022

TANZANIA NA ZAMBIA ZAAZIMIA KUMALIZA CHANGAMOTO ZA KIBIASHARA NA USAFIRISHAJI

Tanzania na Zambia zimedhamiria kumaliza changamoto za kibiashara na usafirishaji zinazowakabili wafanyabiashara ili kuruhusu biashara na usafirishaji wa bidhaa ufanyike bila vikwazo baina ya nchi hizo.

Hayo yamebainishwa katika hotuba ya ufunguzi iliyosomwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine wakati wa Mkutano 10 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika leo tarehe 12 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia.

Balozi Sokoine aliwasisitiza watendaji kutumia mkutano huo kuandaa mikakati ya pamoja itakayosaidia kuondoa vikwazo vya kibiashara na kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta ya umma na binafsi ili ziweze kufanya uwekezaji utakaoleta maendeleo endelevu kwa ajili ya maslahi mapana ya kiuchumi kwa pande zote mbili.

“Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wake wa kindugu na kihistoria na Zambia ili kuendeleza jitihada zilizoasisiwa na waasisi wa mataifa yetu kwa kuweka na mfumo rasmi wa ushirikiano unaowezesha ufuatiliaji wa utekelezaji katika masuala ya ushirikiano” alisema Balozi Sokoine.

Aidha, alieleza kuwa ushirikiano imara na wenye mafanikio ni ule unaojengwa kwa mfumo rasmi ambao unaruhusu kukutana na kufanya majadiliano ya mara kwa mara hivyo, alieleza kuwa ana amini kupitia mkutano huu maeneo yote ya ushirikiano yenye changamoto yatajadiliwa kwa kina kwa maslahi ya nchi zote mbili na wananchi wake.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw. Chembo Mbula alieleza kuwa ni muhimu majadiliano yakaangalia kwa kina maeneo muhimu yatakayowezesha pande zote mbili kuwa na mchango katika maendeleo ya mtangamano wa kikanda.

“Nchi zetu zimepiga hatua kiuchumi na katika maendeleo ya jamii tangu kumalizika kwa mkutano wa tisa wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya ushirikiano baina yetu, hivyo ni vyema majadiliano yakaendana na uhalisia wa mabadilika hayo” alisema, Bw. Mbula.

Pamoja na mambo mengine mkutano huu utapitia na kujadili utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Tisa wa Tume ya Kudumu ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika tarehe 25 na 26 Februari 2016 jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulioanza tarehe 11 Oktoba 2022 kwa ngazi ya Wataalam, utafuatiwa mkutano wa Makatibu Wakuu na utahitimishwa kwa mkutano wa ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 14 Oktoba 2022 jijini humo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw. Chembo Mbula akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Kutoka kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Bw. Ally Gugu na Balozi wa Tanzania nchini Zambia anayemaliza muda wake, Mhe. Hassan Simba Yahya wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.

Ujumbe kutoka Zambia

Ujumbe kutoka Tanzania.

Sehemu nyingine ya ujumbe kutoka Tanzania.

Maafisa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano, kutoka kushoto ni  Bi. Lilian Mukasa na Bw. Makama D. Makamba.

Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kutoka kulia ni Bi. Clementine Msafiri na Bi. Happiness Lyandala wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo.

Ujumbe kutoka Tanzania ukifuatilia ufunguzi wa mkutano, kulia ni Afisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Laila Kagombora.

Ujumbe kutoka Tanzania.

Picha ya Pamoja Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (wa nne kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw. Chembo Mbula (wa tatu kutoka kulia) pamoja na viongozi na maafisa waandamizi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia baada ya hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia unaofanyika kuanzia tarhe 11 hadi 14 Oktoba jijini Lusaka Zambia.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.