Tuesday, October 25, 2022

TANZANIA YAIKUMBUSHA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUISADIA AFRIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Tanzania imeikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza ahadi  yake ya  kuzisaidia kiuchumi nchi za Afrika ili kuziwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya Tabianchini kama makubaliano ya  Mkataba wa Paris  yanavyoelekeza.


Wito huo umetolewa na  Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akihutubia maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 24 Oktoba 2022.



Amesema  Mkataba huo unaitaka Jumuiya ya Kimataifa  kuzisaidia nchi za Afrika katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujenga uwezo, kubadilishana  teknolojia na kuhakikisha nchi hizo  kiuchumi ili kuziwezesha kujitegemea katika kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.



“Wiki mbili zijazo kuanzia leo, Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utafanyika Sharm El Sheikh, Misri. Ni kwa muktadha huo tunahitaji kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba pamoja na mchango mdogo wa Afrika katika ongezeko la joto duniani, bado Afrika ni Bara linaloathirika zaidi na mabadiliko hayo kutokana na uwezo mdogo wa kukabiliana na changamoto hizo. Hivyo, tunaikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kutimiza ahadi kulingana na maelekezo katika  Mkataba wa Paris,’’ amesema Mhe. Dkt. Ndumbaro.



Aidha,  Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kutekeleza program mbalimbali za maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa manufaa ya wananchi.



Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema, Tanzania inapoungana na ulimwengu mzima kuadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa ni kielelezo kinachowakumbusha wadau wote nchini kujiimarisha katika ushirikiano ili kuiwezesha Tanzania kutekeleza pamoja na mambo mengine Mpango wake wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mpango wa Tatu wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.



Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema “Maendeleo Yanayozingatia Ujumuishwaji wa Makundi yote” imebeba ujumbe mzito unaomkumbusha kila mmoja kuungana na kutafuta suluhu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia pasipo kumwacha mtu yoyote nyuma.



Pia amesema Tanzania ipo kwenye hatua za mapitio ya utekelezwaji  wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuwataka wadau mbalimbali kushirikiana nayo ili kufanikisha mapitio hayo.


Vilevile, wakati wa maadhimisho hayo,  Mhe. Dkt. Ndumbaro ameuomba Umoja wa Mataifa kuitambua Lugha ya Kiswahili kama Lugha rasmi ya Umoja huo.



“Tunapoadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa, Tanzania inaikumbusha dunia kuwa wakati umefika sasa wa kuridhia Kiswahili kuwa miongoni mwa Lugha rasmi za Umoja huo” alisema Dkt. Ndumbaro.



Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Kimataifa nchini, Bw. Zlatan Milisic ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi wakimbizi na kwamba Umoja wa Mataifa na Taasisi zake utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo.



Amesema Umoja huo unachangia katika miradi mbalimbali ya  kuwainua kiuchumi wanawake na vijana walio katika mazingira magumu ikiwemo kuchangia katika uunzishwaji wa madawati ya jinsia yaliyo chini ya Jeshi la Polisi ambapo kwa mwaka huu madawati 400 yameanzishwa nchini kote.



Wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Dkt. Ndumbaro alipata fursa ya kuzindua Tovuti ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili.



Maadhimisho hayo ya aina yake yamehudhuriwa na Viongozi na wadau mbalimbali wakiwemo Mhe. Tabia Mwita, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo nchini.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akihutubia wakati wa maadhimisho ya Miaka 77 ya Umoja wa Mataifa. aadhimisho hayo ambayo yalibeba kaulimbiu isemayo "Maendeleo yanayozingatia Ujumuishwaji wa Makundi Yote" yamefanyika kwenye Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam hivi karibuni
Mhe. Dkt. Ndumbaro akiwa na Viongozi wengine walioshiriki maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza na wa tatu kulia ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Mhe. Bw. Zlatan Millisic
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Mhe. Zlatan Milisic akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa
Mhe. Dkt. Ndumbaro akifuatilia Wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa
Mhe. Dkt. Ndumbaro akikagua gwaride la heshima liloandaliwa maalum kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa
Mhe. Dkt. Ndumbaro akishuhudiwa tukio maalum la upandishaji wa Bendera ya Umoja wa Mataifa kama ishara ya kuadhimisha miaka 77 ya Umoja huo

Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia alikuwa Mshereheshaji wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa , Bi. Ellen Maduhu akitoa mwongozo wa maadhimisho hayo kwa washiriki
Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Kibasila ya jijini Dar es Salaam wakitoa burudani na elimu kuhusu historia ya Umoja wa Mataifa kupitia sanaa ya uimbaji
Mhe. Dkt. Ndumbaro akizindua rasmi Tovuti ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili
Picha ya pamoja




 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.