Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema inaendelea kujivunia ushirikiano wake na Serikali ya Watu wa China kwa vitendo zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, (Mb.) katika hafla ya maadhimisho ya miaka 73 ya uhuru wa China iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Katika maadhimishio hayo, Balozi Mulamula na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian, walipanda miti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ikiwa ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya mataifa hayo.
Balozi Mulamula pamoja na mambo mengine, amesema kuwa Tanzania iko tayari kufanya kazi na China ili kuendeleza na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Maendeleo wa Ulimwengu na Mpango wa Usalama wa Ulimwengu katika kuimarisha ushirikiano wa pande zote.
“Tunapoadhimisha miaka 73 ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, tunaadhimisha miaka 61 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi zetu mbili. Tanzania na China ni marafiki wa wakati wote, katika shida na raha,” amesema Balozi Mulamula.
Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Chen Mingjian amesema uhusiano wa China na Tanzania umekuwa ukiendelea kukua kwa kasi na kufikia viwango vya juu kutokana na misingi imara inayosimamiwa na Viongozi wa mataifa haya mawili.
Viongozi wetu, Rais wa China Mhe. Xi Jinping na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wanajali na kuongoza maendeleo ya uhusiano wa mataifa yao kwa maslahi ya pande zote mbili.
“China na Tanzania zimekuwa zikifurahia uhusiano ulioasisiwa na Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa China na Baba wa Taifa hilo Hayati Mao Zedong,” amesema Balozi Mingjean
Balozi Mingjean ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 73 ya uhuru wa China, kumekuwa na ongezeko la miradi ya ushirikiano baina ya China na Tanzania ambapo ongezeko hilo limekuwa chachu ya maendeleo.
Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali zikiwemo, afya, mawasiliano, elimu, uchumi wa kidijitali, biashara na uwekezaji, miundombinu pamoja na utekelezaji wa miradi midogo ya kujikimu kimaisha inayoweza kuwanufaisha wananchi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian wakipanda mti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea katika hafla ya upandaji mti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Picha ya pamoja |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.