Monday, October 17, 2022

TANZANIA KUSHIRIKIANA NA WADAU MBALIMBALI KUBORESHA SEKTA YA MAJI NCHINI

Tanzania ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya maji na usafi wa mazingira nchini ili kuwawezesha wananchi wa mijini na vijijini kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama. 

 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax leo tarehe 17 Oktoba 2022 alipotembelea Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw nchini Poland katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi nchini humo.

 

Mhe. Dkt. Tax ambaye alikutana na Menejimenti ya Chuo hicho pamoja na wamiliki wa kampuni mbalimbali za Poland zenye nia ya kuwekeza katika sekta ya maji nchini, amesema, sekta ya maji na usafi wa mazingira ni miongoni mwa sekta za kipaumbele nchini, kwani zinagusa maisha ya wananchi wote wa mijini na vijijini na kwamba  wanahitajika wawekezaji makini na wenye tija kutoka ndani na nje ya nchi ili kuendelea kuiboresha.

 

Amesema miji mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma na Dar es Salaam inaendelea kukua kwa kasi hivyo upo umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye sekta hiyo ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama lakini pia kuendelea kutunza mazingira.

 

“Maji na usafi wa mazingira ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa   Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali ili kuhakikisha sekta hii inaboreshwa zaidi hususan kwenye teknolojia ya kisasa ya usimamizi wa maji  ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wetu” alisema Dkt. Tax.

 

Pia amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na  Taasisi mbalimbali zinazosimamia sekta ya maji nchini ikiwemo Wizara ya Maji ili kwa pamoja kuendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo kwa kuwashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi.

 

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri chuoni hapo, Mkuu wa Chuo, Prof. Michal Zasada amesema chuo hicho ambacho kimejikita katika ufundishaji wa Teknolojia mpya ya usimamizi wa maji na utunzaji wa mazingira, kipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam wa sekta hiyo kutoka nchini.

 

“Tumefarijika kutembelewa na wewe Mhe. Waziri na ujumbe wako kutoka Tanzania. Chuo chetu kinatoa kozi mbalimbali za Shahada na Shahada ya Uzamili katika masuala mbalimbali ikiwemo sekta ya maji. Tayari wataalam kadhaa kutoka sekta ya maji wamewahi kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo hapa chuoni. Tunaendelea kuwakaribisha Watanzania kujiunga na program mbalimbali za mafunzo hususan za sekta ya maji zinazotolewa chuoni hapa” alisema Prof.  Zasada.

 

Wakati wa Mkutano huo Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na sekta ya maji na usafi wa mazingira za Poland ikiwemo ile ya Asseco ziliwasilisha mada na kueleza utayari wao wa kuwekeza katika sekta ya maji kwa kuanza na miji ya Dodoma na Dar es Salaam.

 

Akiwa chuoni hapo Mhe. Dkt. Tax alipata fursa ya kutembelea maabara za kisasa za usimamizi wa maji pamoja na  kujionea mradi wa maji unaotumia teknolojia ya kisasa unaotekelezwa na chuo hicho.

 

Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Maisha cha Warsaw nchini Poland, Prof. Michal Zasada mara baada ya kuwasili Chuoni hapo leo tarehe 17 Oktoba 2022. Pamoja na ambo mengine Mhe. Waziri Tax alizungumza na menejimenti ya chuo hicho kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta ya elimu na maji pamoja na kutembelea miradi ya maji inayotekeelzwa na chuo hicho. Mhe. Dkt. Tax yupo nchini poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2022


Mhe Waziri Dkt. Tax akizungumza na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw cha nchini Poland kuhusu masuala ya ushirikiano katika sekta za elimu na maji. Kushoto kwake ni Prof. Zasada, Mkuu wa Chuo hicho akifuatiwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Marta Mendel na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Mhe. Krystof Buzalski. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani anayewakilisha pia nchini Poland, Mhe. Balozi Abdallah Possi
Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, Prof. Zasada akizungumza kumkaribisha Mhe. Dkt Tax alipotembelea Chuoni hapo

Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (kulia) akiwa pamoja na Wajumbe kutoka Tanzania walioambata na Mhe. Waziri Tax nchini Poland.

Sehemu ya Wajumbe kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw na wamiliki wa Kampuni zinazojishughulisha na masuala ya maji wakifuatilia kikao
 
Sehemu nyingine ya Wajumbe kutoka Tanzania
 
Sehemu ya washirki kutoka Chuoni hapo
Sehemu ya Washiriki kutoka Tanzania
 
Mkutano ukiendelea
 
Sehemu ya wajumbe kutoka Chuoni hapo
 
Sehemu nyingine ya washiriki
 
Mada kuhusu masuala ya maji na usafi wa mazingir aikiwasilishwa na mmoja wa washiriki kutoka Poland
 
Mhe. Dkt. Tax akimweleza Prof. Zasada kuhusu zawadi  kutoka Tanzania kabla ya kumkabidhi. Zawadi hiyo ni mkusanyiko wa bidhaa za Tanzania zikiwemo Kahawa, Korosho, batiki, Vikoi na Viungo vya chakula.
 
 
Prof. Zasada naye akimkabidhi zawadi Mhe. Waziri Dkt. Tax
Picha ya pamoja
Mhe. Dkt. Tax akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kituo cha Maji kilicho chini ya Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, Prof. Wojciech Sas alipofika kukitembelea kituo hicho na kujionea maabara mbalimbali za maji

Mhe. Dkt Tax na ujumbe wake wakipata maelezo kutoka kwa mtaalam wa mitambo na teknolojia mbalimbali za maji Prof. Adam Kiszko


Mhe. Dkt. Tax akipata maelezo kutoka kwa mtaalam wa maabara ya maji alipotembelea maabara hiyo

Mhe. Dkt. Tax akiangalia bwawa lililochimbwa kitaalam bila kuharibu mazingira na viumbehai  alipotembelea Kituo cha Maji kilicho chini ya Chuo Kikuu cha Sayansi za maisha cha Warsaw, Poland




 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.