Sunday, October 23, 2022

TANZANIA YAJIVUNIA USHIRIKIANO IMARA NA UMOJA WA MATAIFA

Tanzania imesema inajivunia ushirikiano kati yake na Umoja wa Mataifa (UN) na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo katika kuendeleza programu mbalimbali za maendeleo endelevu.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo maadhimisho hayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 24 Oktoba.

“Tanzania inanufaika na uanachama wake kwenye Umoja wa Mataifa katika maendeleo. Kwa mfano, kupitia Mpango wa Malengo ya Milenia na Malengo ya Maendeleo Endelevu. Umoja wa Mataifa unaendelea kusaidia nchi wanachama kutekeleza malengo hayo ili kukuza amani, utawala wa sheria, haki za binadamu na maendeleo kwenye sekta mbalimbali. Tanzania imekuwa mnufaika wa mikakati hiyo na  mwezi Mei, 2022, Umoja wa Mataifa ulizindua mpango wake mpya wa ushirikiano unaojulikana kwa jina la United Nations Sustainable Development Cooperation Framework baina ya Tanzania na Umoja huo, unaolenga kuleta maendeleo kwenye maeneo mbalimbali nchini,” alisema Balozi Mbarouk.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini inasaidia kuhamasisha wadau mbalimbali kama vile taasisi za Serikali, asasi za kiraia, wanataaluma na kadhalika kupitia programu zake ili kuleta maendeleo ya Watanzania kama vile kuboresha huduma za afya, kutokomeza umaskini, njaa, kuhuisha sekta ya elimu, kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na kukuza sayansi na teknolojia.

“Manufaa mengine ni ajira kwa Watanzania kwenye taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa pamoja na misheni za kulinda amani za Umoja huo, suala linalonufaisha maisha ya Mtanzania mmoja mmoja lakini pia Taifa kwa ujumla,” Aliongeza Balozi Mbarouk.

Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan Milišić amesema Umoja wa Mataifa umelenga kusaidia watu, ustawi, dunia na mazingira ili kuwawezesha wananchi kufikia vipaumbele vya maendeleo ya taifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). 

“Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake kwa kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa unaahidi kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada za maendeleo za Serikali ili kuiwezesha kufikia vipaumbele vyake vya maendeleo na SDGs,” amesema Bw. Milišić. 

Mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani anatarajia kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.)

Maadhimisho rasmi ya Siku ya Umoja wa Mataifa yatafanyika rasmi tarehe 24 Oktoba 2022 katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya madhimisho ya mwaka huu ni “Maendeleo yanayozingatia ujumuishwaji wa makundi yote”.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan Milišić. 

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan Milišić akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk pamoja na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan Milišić wakizungumza na waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.