Sunday, October 23, 2022

TANZANIA, DRC ZAKUBALIANA KUIMARISHA BIASHARA NA UCHUMI

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inaedelea kuudhirihishia ulimwengu kuwa imedhamiria kushirikiana na wadau wote, zikiwemo nchi jirani ili kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote.

Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) nchini, Mhe. Felix Tshisekedi ambayo ni mwendelezo wa ziara kadhaa za viongozi wa kitaifa na mashirika ya kimataifa nchini ni kielelezo cha wazi cha kutambua nguvu ya ushirikiano katika kukuza uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla.

Rais Samia na mgeni wake, Rais Tshiseked katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar Es Salaam tarehe 23 Oktoba 2022, waliafikiana nchi zao ziongeze nguvu kuimarisha ushirikiano katika sekta za kiuchumi, miundombinu, biashara, usafirishaji, uwekezaji, ulinzi, usalama na mawasiliano.

Rais Samia aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekubaliana kuondoa vikwazo vyote visivyo vya kibishara ili kukuza biashara na kwamba mawaziri wa biashara wa pande zote mbili wameagizwa  kulifanyia kazi suala hilo haraka iwezekanavyo. 

"Ikumbukwe DRC ni mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika mikakati ya kuendeleleza miundombinu ya Jumuiya hiyo, kuna mpango wa kujenga ushoroba wa kati utakaounganisha Tanzania na DRC ili kukuza biashara na mtangamano baina ya nchi wanachama', alisema Rais Samia.

Kwa upande wake, Rais Tshisekedi alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama kwa sababu bila ya amani na usalama hakuna miradi itakayoweza kutekelezwa

“Sisi kwetu DRC usalama ni muhimu sana na ndiyo maana mimi kama Rais nimeweka mkazo wa kujenga na kuimarisha uhusiano wa kindugu na majirani zetu,” alisema Rais Tshisekedi.

Rais Samia na mgeni wake walishuhudia uwekaji saini wa Mkataba wa Teknolojia ya Habari na Posta uliosainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Mhe. Christophe Lutundula.

Uwekaji saini wa mkataba huo umekuja muda mfupi baada ya nchi hizo pia kusaini Hati ya Makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama wakati wa Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya nchi hizo uliofanyika Jijini Dar Es Salaam mwezi Septemba 2022. Ikumbukwe pia Rais Samia alifanya ziara ya kitaifa nchini DRC mwezi Agosti 2022 mara baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika nchini humo ambapo Rais Tshesiked alikabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Ziara hii ya Rais wa DRC na nyingine zilizofanywa na viongozi wa ngazi tofauti baina ya nchi hizi mbili pamoja na uamuzi wa Tanzania wa kufungua Ofisi ya Konseli Kuu katika mji wa Lubumbashi vinatajwa kuwa vitaimarisha uhusiano na kukuza biashara baina ya mataifa hayo mawili yenye utajiri mkubwa wa maliasili.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi wakishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Teknolojia ya Habari na Posta uliosainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Mhe. Christophe Lutundula Ikulu Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax akifuatilia Mkutano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi na waandishi wa Habari uliofanyika Jijini Dar es Salaam




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.