Saturday, October 15, 2022

TANZANIA NA ZAMBIA ZASAINI MKATABA WA KUBADILISHANA WAFUNGWA NA MKATABA WA UTATU WA CHEMBA ZA BIASHARA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia zimesaini Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa na Mkataba wa Utatu kati ya Chemba za Biashara za nchi hizo wakati wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri uliomalizika tarehe 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka.

Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa ulisainiwa kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kabubo.

Wakati huo huo, Mkataba wa Utatu kati ya Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) na Chemba ya Taifa ya Biashara ya Zanzibar (ZNCC) za Tanzania na Chemba ya Wafanyabiashara na Viwanda (ZACCI) ya Zambia ulisainiwa na Rais wa TCCIA, Bw. Paul Koyi na Mtendaji Mkuu wa TCCIA na Bw. Nerbat Mwapwele kwa niaba ya Mwenyekiti wa ZNCC. Pia kwa upande wa Zambia mkataba huo ulisainiwa na Mtendaji Mkuu wa ZACCI, Bw. Phil Daka.

Aidha, Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri, ulitanguliwa na mkutano katika ngazi ya wataalam uliofanyika tarehe 11 na 12 Oktoba 2022 na kufuatiwa na Mkutano katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe  13 Oktoba 2022. 

Pamoja na mambo mengine mkutano huo pia ulitathimini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema aliyofanya nchini Tanzania mapema mwezi Agosti 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kulia) akihutubia wakati wa kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika tarehe 11 hadi 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Stanley Kabubo wa Zambia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Stanley Kabubo wa Zambia wakisaini Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa kati ya nchi zao leo tarehe 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Kabubo wakionesha Hati zilizosainiwa kwa wajumbe wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Kabubo wakishuhudia Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Bw. Paul Koyi na Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Wafanyabiashara na Viwanda, Bw. Phil Daka wakisaini mkataba  wa ushirikiano kati ya chemba hizo.

Mtendaji Mkuu wa TCCIA, Bw. Nerbat Mwapwele akisaini Mkataba wa ushirikiano wa Chemba za Biashara kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya Biashara ya Zanzibar (ZNCC) utiaji saini huo pia ulishuhudiwa na Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Kabubo.

Kulia Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Naibu Waziri Wizara ya  Ujenzi na Uchukuzi, Bw. Atupele Mwakibete wakifuatilia hafla ya kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Kutoka Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Bw. Ally Gugu wakifuatilia hafla ya kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Kutoka Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia anayemaliza muda wake, Mhe. Hassan Yahya Simba na Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia hafla ya kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimpa zawadi ya picha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kabubo.




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.