Hati hiyo, imesainiwa
tarehe 21 Oktoba 2022 jijini Lisbon kati
ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno, Mhe. João Gomes Cravinho.
Akizungumza wakati
wa mazungumzo rasmi kati yao, Mhe. Dkt. Tax amesema anaishukuru Serikali ya
Ureno na Serikali yake kwa hatua hii muhimu katika ushirikiano wa kidiplomasia na
kwamba kusainiwa kwa hati hiyo kunalenga kuupeleka ushirikiano huo katika hatua
nyingine ya juu ambapo nchi hizi mbili zitaongeza zaidi ushirikiano katika
maeneo mbalimbali yenye maslahi kwao ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, uchumi wa
buluu, usafirishaji na elimu.
Vilevile amesema kwamba
hii ni ishara kwamba nchi hizi mbili zina nia ya ya dhati ya kushirikiana kwenye
masuala mbalimbali ya manufaa kwa pande zote mbili.
“Ziara yangu nchini
Ureno imekuwa ni ya manufaa makubwa kwani kwa mara ya kwanza katika historia ya
ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hii tumesaini Hati ya Makubaliano ya
kuanzisha majadiliano ya kisiasa baina yetu. Hii ni hatua ya juu katika
ushirikiano wa kidiplomasia kwani sasa masuala mengi ya ushirikiano kati yetu ikiwemo
biashara, uwekezaji, utalii, yataimarika na kwenda viwango vingine vya juu kwa manufaa
ya pande zote mbili”, alisema Dkt. Tax.
Ameongeza kusema
kuwa, wamekubaliana na Waziri mwenzake kuweka mikakati thabiti ya pamoja ya ufuatiliaji
wa utekelezaji wa maeneo mbalimbali ya
ushirikiano waliyokubaliana ambapo pia Mhe. Dkt. Tax amewataka Watanzania kutumia
hatua ya kusainiwa kwa mkataba huo kama chachu ya kuanza kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo Ureno ikiwemo
biashara kwa bidhaa za kahawa, chai, samaki, viungo vya chakula na mbao.
Pia, wakati wa mazungumzo yao, Tanzania imesisitiza
umuhimu wa nchi hiyo kushirikiana nayo katika medani za kimataifa hususan
kuendelea kupaza sauti ili nchi za Ulaya ziendelee kuisadia Tanzania na nchi za Afrika katika kukabiliana na
changamoto zinazotokana na mabadiliko ya
Tabianchi.
Kwa upande wake, Mhe.
João Gomes Cravinho amemshukuru Mhe. Dkt. Tax kwa kukubali
mwaliko wake na kutembelea nchini humo na kwamba Ureno inathamini mchango wa
Tanzania kupitia ushirikiano uliopo kati yao ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika
medani za Kimataifa.
Amesema ana imani kuwa kusainiwa kwa Hati hiyo
muhimu ni mwanzo mpya wa ushirikiano huo ambapo nchi hizi mbili sasa
zitazingatia na kujitoa zaidi katika kuhakikisha ushirikiano uliopo unaimarika
zaidi.
“Hatua ya kusainiwa kwa Hati hii ni ya
kihistoria.. Kilichobaki sasa ni kuhakikisha yale tuliyokubaliana leo na
kupitia hati hiyo yanatekelezwa” alisema Mhe. Gomez.
Akizungumzia maeneo ambayo nchi hiyo imepiga
hatua na ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuwa ni pamoja na eneo la Nishati
Mbadala. Alisema nchi hiyo hadi sasa imefikia asilimia 62 ya matumizi ya
Nishati hiyo na kwamba malengo yao ni kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2026.
Wakati wa mazungumzo
yao viongozi hao pia walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika masuala ya
biashara, elimu, utalii, sanaa na michezo pamoja na kukuza Lugha ya Kiswahili
kwa upande wa Ureno na Kireno kwa upande wa Tanzania.
Ziara ya Mhe. Waziri Tax nchini Ureno ni matokeo ya majadiliano kati ya Rais wa Ureno, Mhe. Rebelo De Sousa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Isdor Mpango walipokutana mwezi Juni 2022 pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari ambapo walizungumza kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Mhe. Dkt. Tax amehitimisha ziara yake ya siku mbili aliyoifanya nchini humo kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba 2022 kwa mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. João Gomes Cravinho. Itakumbukwa kuwa, Mhe. Waziri Tax alianza ziara yake nchini Poland kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2022 kabla ya kutembelea Ureno.
Waheshimiwa Mawaziri wakibadilisha Hati hiyo muhimu mara baada ya kusaini |
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes wakionesha Hati hiyo mara baada ya kusaini |
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes wakiwa katika mazungumza rasmi kuhusu namna ya kuimarisha na kuboresha ushirikiano kati ya Tanzania na Ureno |
Maafisa kutoaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakinukuu mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes. Kushoto ni Bi. Liliani Kimaro na Bi. Sekela Mwambegele. |
Mhe. Gomes akimkabidhi zawadi Mhe. Dkt. Tax mara baada ya kukamilisha mazungumzo rasmi |
Mhe. Dkt. Tax naye akimpatia zawadi Mhe. Gomes. Zawadi hiyo ni bidhaa za Tanzania ikiwemo Korosho, Kahawa, Asali, Batiki na Viungo vya Chakula |
Mhe. Gomes akimtambulisha Mhe. Dkt. Tax kwa wasaidizi wake |
Ujumbe wa Tanzania |
Mkuu wa Itifaki wa Ureno akisoma Hati ya Makubaliano kwa Mawaziri kabla ya kusainiwa |
Mhe. Dkt. Tax na mwenyeji wake Mhe. Gomes wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha mazungumzo kati yao |
Mhe. Dkt. Tax akiagana na Mhe. Gomes mara baada ya kukamilisha mazungumzo na kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano |
Picha ya pamoja |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.