Tanzania imefanikiwa kushinda kwa
kishindo katika uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Shirika la Mawasiliano Duniani
(ITU) katika uchaguzi uliofanyika wakati wa mkutano mkuu wa ITU jijini
Bucharest, Romania leo, tarehe 3 Oktoba 2022. Tanzania imepata kura 141 kati ya
kura 180 zilizopigwa na nchi wanachama wa Shirika hilo.
Baraza la ITU husimamia shughuli za
Shirika katika kipindi cha kati ya mikutano mikuu ambayo hufanyika kila baada
ya miaka 4.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu
uliongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Mnauye (Mb) na kujumuisha maofisa waandamizi wengine kutoka Wizara ya
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mashirika na Taasisi za Mawasiliano nchini.
Kwa kuchaguliwa kwake, Tanzania sasa
itakuwa mjumbe wa Baraza la ITU kwa kipindi cha miaka 4 ijayo. Ushindi huu ni
mafanikio makubwa kwa Tanzania na ni kielelezo cha kazi nzuri anayoifanya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan katika medani ya
kimataifa na hivyo kuifanya nchi iweze kukubalika na kuaminiwa.
Ushindi huu pia ni matokeo ya kampeni
ya kimkakati iliyoendeshwa na Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa
Mataifa - Geneva. Aidha, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
na Taasisi zilizopo chini yake zilizifanya kazi kubwa ya kampeni na kutoa
raslimali muhimu kwa ajili hii.
Itakumbukwa kuwa Tanzania iliwahi kuwa
mjumbe wa Baraza hili kabla ya kushindwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka
2018, Dubai UAE.
Miongoni mwa faida za kuwa mjumbe wa
Baraza la ITU ni pamoja na:
• Kuwa katika nafasi nzuri ya
kutambua fursa zilizopo na hatimaye kunufaika na misaada na huduma zinazotolewa
na Mashirika na pia kupata taarifa muhimu za miradi na shughuli za ITU kwa
urahisi na haraka
• Kujua na kuratibu mwenendo wa
teknolojia mpya ili kuandaa njia za utatuzi wa changamoto zake.
• Kukuza uwezo wa kiutendaji wa
wataalamu nchini wanaoshiriki katika shughuli za Baraza ikiwa ni pamoja na
kubadilishana ujuzi na uzoefu na nchi nyingine katika masuala mbalimbali.
• Kupata fursa ya kupokea na
kuchambua taarifa mbalimbali za utendaji wa ITU, kutoa mapendekezo na kuboresha
mwenendo wa Umoja.
• Kuwasilisha mapendekezo ya nchi juu
ya uendeshaji wa ITU.
• Kushawishi maamuzi yatolewayo na
Baraza yasiwe na matokeo hasi kwa sekta ya mawasiliano.
• Kuitangaza nchi na kuchangia
maendeleo ya sekta ya mawasiliano barani Afrika na duniani kwa ujumla. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.