Tuesday, October 25, 2022

KATIBU MTENDAJI WA SADC AFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI

Tanzania itaendelea kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)ili kufikia malengo ya kukuza uchumi na kudumisha amani na usalama katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.



Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokutana kwa mazungumzo na Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Mpedi Magosi wakati wa ziara yake ya kikazi nchini hivi karibuni.



Mhe. Dkt. Tax amesema lengo kuu la Jumuiya hiyo ni kuziwezesha kujikomboa kiuchumi nchi za Kusini mwa Afrika. Lakini pia kuhakikisha nchi za ukanda huo zinakuwa na amani na utulivu, hivyo Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi zozote zinazofanywa na Sekretarieti hiyo ili kufikia malengo hayo.



Pia alivitaja vipaumbele vya Tanzania kwenye Jumuiya hiyo kuwa ni pamoja na Amani na Usalama, Kilimo, Uchumi wa Buluu, maendeleo ya Miundombinu na uchumi  wa kidigitali.



Ameongeza kusema kazi kubwa ya Sekretarieti hiyo ni kusimamia kwa bidii utekelezaji wa mipango, itifaki, na mikataba mbalimbali iliyokwishapitishwa au kuridhiwa na nchi wanachama.


"Nakushukuru sana kwa kutenga muda wako na kuja kutembelea Tanzania. Nakupongeza pia kwa kazi nzuri unayoendelea kufanya ya kuongoza chombo muhimu kinachosimia utekelezaji wa malengo ya Jumuiya yetu. Ushauri wangu kwako ni kuendelea kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali ambayo tayari yapo kwa ajili ya utekelezaji" alisema Mhe. Dkt. Tax.



Kadhalika alimkumbusha Mhe. Magosi kuendeleza jitihada za kutangaza majukumu na umuhimu wa Jumuiya hiyo katika Nchi Wanachama kwani bado Agenda na Madhumuni ya Jumuiya hayajulikani ipasavyo miongoni mwa wananchi katika Nchi Wanachama.

 

Kwa upande  wake, Mhe. Magosi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Dkt. Tax kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo mpya na kumuahidi ushirikiano wake binafsi na kutoka katika Sekretarieti. Pia alimpongeza kwa uongozi makini wa miaka nane kama Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC  hususan katika uandaaji wa nyaraka ikiwemo  Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC wa mwaka 2020-2030.



Pia aliipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ugaidi na kwamba uwepo wa kituo hicho hapa nchini kunadhihirisha utayari wa Tanzania katika kuhakikisha suala la usalama katika kanda linapewa kipaumbele.



Wakati wa ziara hiyo ya siku mbili hapa nchini kuanzia tarehe 24 hadi 25 Oktoba, 2022, Mhe. Magosi amekutana kwa mazungumzo na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametembelea Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ugaidi pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD). 

 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Mhe. Elias Masego alipomtembelea jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Mhe. Masego yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 24 hadi 25 Oktoba 2022.
Mhe. Masego akizungumza wakati wa kikao kati yake na Mhe. Dkt. Tax
Ujumbe uliofuatana na Mhe. Masego wakifutilia kikao

Ujumbe wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola (kushoto) wakifuatilia mazungumzo
Mhe. Masego akimpatia zawadi Mhe. Dkt. Tax

Picha ya pamoja
Mhe. Masego akizunguza wakati alipotembelea Kituo cha Kikanda cha SADC cha Kupambana na Ugaidi kilichopo Dar es Salaam

Mhe. Masego alipotembelea Kituo cha Kikanda cha SADC cha Kupambana na Ugaidi 
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Kayola (kushoto) wakati wa ziara ya Mhe. Masego kwenye Kituo cha Kupambana na Ugaidi 
Kikao kikiendelea
Kaimu Mkurugenzi wa Bahari Kuu ya Dawa (MSD), Bw. Leopold Shayo akizungumza wakati wa ziara ya Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Masego kwenye Bohari hiyo. Kushoto ni Mhe. Masego akimsikiliza. Mhe. Masego ametembelea Bohari hiyo kutokana na kushinda zabuni ya kusambaza dawa na vifaa tiba kwa nchi za SADC
Kikao kati ya Mhe. Masego na MSD kikiendelea
Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Bw. Shayo akimsikiliza Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Masego (hayupo pichani)
Mhe. Masego akizungumza alipotembelea MSD
Mazungumzo yakiendelea

Mhe. Maseko akipokea zawadi ya barakoa zinazotengenezwa na MSD kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Bw. Shayo. 
Picha ya pamoja




























 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.