Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Dkt. Stergomena Tax amekutana na kufanya kikao na watumishi wa Ubalozi wa
Tanzania nchini Zambia tarehe 13 Oktoba 2022 katika ofisi za ubalozi huo Jijini
Lusaka, Zambia.
Mhe. Tax amekutana na watumishi wa Ubalozi huo baada ya
kuwasili nchini Zambia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja
ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Mawaziri utakaofanyika
tarehe 14 Oktoba 2022.
Akiongea katika kikao na watumishi hao Mhe. Waziri Tax
ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ni wa kihistoria na kidugu
uliojengwa kupitia ujirani mwema na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Mataifa
hayo mawili Hayati Baba wa Taifa la Tanzania Mw. Julius Kambarage Nyerere na
Hayati Keneth Kaunda wa Zambia. Kupitia kikao hicho, Mheshimiwa Waziri Tax
ameelekeza Ubalozi kuendelea kuwa kiungo katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano
wa kiuchumi na kijamii kwa kufuata misingi iliyowekwa na Waasisi wa Mataifa
hayo.
“Fanyeni kazi kwa bidii hususan wakati huu tunapotekeleza
diplomasia ya uchumi ili ushirikiano wetu uweze kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa
maslahi mapana ya nchi yetu”alisema Mhe. Waziri Tax.
Naye Balozi wa Tanzania nchi Zambia anayemaliza muda wake
Mhe. Hassan Yahya Simba akisoma taarifa ya utekelezaji, ameeleza kuwa ubalozi
unaendelea kusimamia ushirikiano wa mataifa hayo mawili kwa kuhakikisha
unafatilia kwa karibu maslahi ya Taifa na maslahi ya Watanzania wanaoishi na
kuingia nchini Zambia kwa shughuli mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt. Tax ametumia nafasi hiyo
kutembelea majengo yanayomilikiwa na ubalozi wa Zambia pamoja na ofisi za Mamlaka
ya Usimamizi wa Bandari (TPA) zilizopo jijini Lusaka, Zambia.
Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia umekuwa ofisi ya kwanza ya
uwakilishi kutembelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.
Maafisa wa Ubalozi wakifuatilia kikao hicho. |
Picha ya pamoja. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.