Tuesday, March 31, 2020

PROF. KABUDI ATEMBELEA IDARA NA VITENGO WIZARANI AZUNGUMZA NA WATUMISHIWaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof.  Palamagamba John Kabudi (wa kwanza kulia) akizungumza na watumishi wa Idara ya Ulaya na Amerika wakati alipowatembelea na kujadililiana nao masuala mbalimbali ya utendaji kazi wa Idara hiyo kwenye ofisi za Wizara zilizopo Chuo Kikuu cha Dodoma, tarehe 31 Machi 2020

Mhe. Waziri Prof. Kabudi akimsikiliza mmoja wa watumishi wa Idara ya  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakitoa ufafanuzi kuhusiana na utekelezaji wa majukumu ya idara.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof.  Palamagamba John Kabudi ametembelea Idara na vitengo vya wizarani na kuzungumza na watumishi walioko katika ofisi za wizara
kwenye majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma, tarehe 31 Machi 2020.

Prof. Kabudi ametumia nafasi hiyo kuzungumza na mtumishi mmoja mmoja ili kuwafahamu na kuona jinsi  wanavyoyafahamu na kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuona namna wanavyogeuza changamoto wanazokutana nazo kuwa fursa katika sehemu zao za kazi


KATIBU MKUU BALOZI KANALI IBUGE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA NCHINI KWA NJIA YA VIDEO

KATIBU MKUU BALOZI KANALI IBUGE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA NCHINI KWA NJIA YA VIDEO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akiwa Dodoma, terehe 30 Machi 2020 amefanya mazungumzo kwa njia ya video (video conference) na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke. 
                                                        
Pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya mahusiano ya pande mbili (bilateral relations), viongozi hawa walizungumzia utayari wa Serikali wa nchi zote mbili katika kupambana na mgonjwa wa COVID-19. Sambamba na utayari huo, Katibu Mkuu alimfahamisha Balozi Wang Ke kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na kuenea  kwa ugonjwa wa virusi vya corona. Wakati huohuo, alimweleza kuhusu utayari wa Serikali kushirikiana na wadau wengine duniani ikiwemo China katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona. 

Vilevile, Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, kwa jitihada kubwa walizozifanya kiasi cha kufanikiwa kudhibiti kuenea zaidi kwa COVID-19 nchini humo na jitihada wanazozifanya ikiwemo kusaidia wataalamu, vifaa  tiba na vya kujikinga kwa Mataifa mengine duniani ambapo COVID-19 inaendelea kuleta madhara. Hadi sasa China imefanya mazungumzo na nchi 24 za Afrika ikiwemo Tanzania yanayolenga kushauri na kubadlishana uzoefu na taarifa muhimu zitakazo saidia kutokomeza COVID-19. 

Aidha,katika mazungumzo hayo Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke amebainisha kuridhishwa kwake juu ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona. Balozi Wang Ke aliongezea kusema pamoja na kutokuwepo maambukizi mapya nchini China, Serikali ya nchi hiyo bado inaendelea kuchukua tahadhari na hatua za kuzuia maambukizi mapya, na  kuwa wataendelea kutoa mchango kwa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na COVID-19. Balozi Wang Ke amesisitiza kuwa, Serikali ya China ipotayari kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya COVID-19.

Katibu Mkuu ameushukuru Ubalozi wa China kwa utayari wake wa kushirikiana na Tanzania dhidi ya mapambano ya COVID-19, na kueleza kwamba Wizara itawasiliana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ili kuandaa orodha ya mahitaji ambayo Ubalozi wa China unaweza kusaidia. Katibu Mkuu alirejea kauli ya Serikali kwamba mapambano dhidi ya virusi vya corona ni vita ambayo Tanzania haina budi kukabiliana navyo, kwa ujumla wake na kwamba hatua zote ambazo Tanzania inachukua chini ya uongozi wa Waziri Mkuu zinalenga kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo bila kuathiri shughuli za kila siku.  Alisistiza kwamba Tanzania inaamini kwa jitihada inazochukua na kwa ushirikiano kutoka China itafanikiwa kushinda janga hili.

Mwisho, Balozi Wang Ke alimpongeza Katibu Mkuu kwa kuendelea kufanya mikutano na Waheshimiwa Mabalozi licha ya changamoto iliyopo ya COVID-19 kwa kuweka utaratibu wa kufanya kwa mikutano hiyo kwa njia ya Video akiwa Ofisini kwake Mtumba, Dodoma wakati Mabalozi wakiwa Dar es Salaam. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akifafanua jambo wakati wa mazungumzo yaliyofanyika kwa njia video na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke. Katibu Mkuu Balozi Kanalı Ibuge amefanya mazungumzo hayo akiwa Ofisini kwake Mtumba, Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akimsikiliza Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke walipofanya mazungumzo kwa njia ya video. Machi 30, 2020
Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke akielezea jambo wakati wa mazungumzo kwa njia ya video na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge. Balozi wa China nchini Mhe.Wang Ke amefanya mazungumzo hayo akiwa Dar es Salaam.
Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke akimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge walipofanya mazungumzo kwa njia ya video tarehe 30 Machi 2020.

Thursday, March 26, 2020

TAARIFA


KATIBU MKUU BALOZI KANALI IBUGE AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA VIETNAM

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Balozi Col. Wilbert A. Ibuge katikati akimkaribisha Balozi wa Vietnam chini Mhe. Nguyen Kim Doanh katika ofisi za Wizara  Jijini Dodoma alipofika kuitikia wito wa Katibu Mkuu kulia ni Kaimu Mkurugenzi anayeshughulikianchi za Asia na AustralasiaBw. Ceasar Waitara.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Balozi Col. Wilbert A. Ibuge (kulia) akizungumza na Balozi wa Vietnam chini Mhe. Nguyen Kim Doanh katika ofisi za Wizara  Jijini Dodoma alipofika kuitikia wito wa Katibu Mkuu

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Balozi Col. Wilbert A. Ibuge (kulia) akizungumza na Balozi wa Vietnam chini Mhe. Nguyen Kim Doanh katika ofisi za Wizara  Jijini Dodoma alipofika kuitikia wito wa Katibu Mkuu

Balozi wa Vietnam chini Mhe. Nguyen Kim Doanh (katikati) akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Balozi Col. Wilbert A. Ibuge (kulia) alipofika katika ofisi za Wizara  Jijini Dodoma kuitikia wito wa Katibu Mkuu kushoto ni afisa ubalozi wa Vietnam aliyefuatana na Mhe. Balozi Nguyen.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Wilbert Ibuge na Balozi Nguyen Doanh wa Vietnam wakiangalia nyaraka mbalimbali walipokutana Ofisini jijini Dodoma kuzungumzia namna ya kuimarisha na kuboresha mahusiano ya kihistoria yaliyopo baina ya Tazania na Vietnam.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Wilbert Ibuge na Balozi Nguyen Doanh wa Vietnam wakiagana walipomaliza mazungumzo yao Ofisini jijini Dodoma .


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Balozi Col. Wilbert A. Ibuge leo tarehe 26 Machi, 2020 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Kim Doanh katika ofisi za Wizara, Makao Makuu, Jijini Dodoma.

Balozi Doanh alikuja jijini Dodoma kufuatia wito wa Balozi Ibuge na kufanya mazungumzo yaliyohusu mambo mbalimbali kuhusu mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam, likiwemo suala la uwekezaji wa Vietnam nchini kupitia Kampuni ya simu ya Halotel. 

Katika mazungumzo yao,  viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya Nchi mbili hizo, ikiwemo uendelevu wa mawasiliano ya Kidiplomasia ambapo mahusiano ya Tanzania na Vietnam yamefikisha miaka 55 mwaka huu huku  fursa za uwekezaji nchini zikiendelea kuimarishwa na hivyo kuiwezesha Serikali ya Vietnam ambayo ni mmiliki wa Kampuni ya Simu ya mkononi ya Halotel kuwekeza nchini na kuendesha shughuli zake.  

  
Balozi Ibuge pia alimjulisha Mhe. Balozi Doanh kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara itaendelea kuhimiza uwekezaji kutoka Vietnam na kusisitiza uwekezaji huo  kuzingatia sheria za nchi, kwa lengo la kuwepo tija kwa pande zote zinazohusika. 

Kufuatia kikao hicho, Mhe. Balozi Doanh aliahidi kuendelea kuyasisitiza makampuni ya Vietnam Nchini ikiwemo kampuni ya Halotel kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika.