Waziri wa wa Mambo ya Nje wa Nepal, Mhe. Pradeep Gyawali
alifungua rasmi ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal katika hafla
iliyofanyika katika Hoteli ya Radisson Jijini Kathmandu tarehe 02 Machi 2020.
Katika hotuba yake, Waziri Gyawali alieleza kuridhishwa kwake
kutokana na uhusiano thabiti wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili
ambapo zinashirikiana na kujenga hoja zinazofanana kwenye medani ya Umoja wa
Mataifa, Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote, Kundi la 77 na
nyinginezo.
Hata hivyo, Waziri Gyawali alielezea umati wa washiriki katika
hafla hiyo kuwa kwa sasa, uhusiano huu unapaswa kujikita zaidi katika maeneo
ambayo mbia mmojawapo anaweza kunufaika na ujuzi na uzoefu kutoka kwa mwenzake.
Akataja maeneo ambayo Nepal imefanikiwa zaidi kama vile utalii wa kupanda
milima ambapo Nepal inavyo vilele vya milima nane mirefu kuliko yote duniani
ikiongozwa na Mlima Everest.
Awali akimkaribisha Mheshimiwa Waziri Gyawali, Balozi Baraka
Luvanda anayeiwakilisha Tanzania nchini India na Nepal alielezea juu ya umuhimu
wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima kuwa itasaidia kutoa huduma za Kikonseli kwa
karibu zaidi na pia itasaidia kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili.
Balozi Luvanda alitaja maeneo ambayo yanaweza kutazamwa kama ya
kuanzia kama vile (i) Kuwa na Makubaliano ya Mashauriano ya Kisiasa (Political
Consultations) (ii) Kuwa na Makubaliano katika Sekta ya Usafiri wa Anga
(Bilateral Air Services) ambapo “Air Tanzania” inaweza kuingia ubia na “Nepal
Airline” (iii) Kuwa na Makubaliano kwenye sekta ambazo Nepal inafanya vizuri
kama vile Utalii wa kupanda milima na Kilimo.
Bwana Rajesh Chaudhary, raia wa Nepal amekwishaanza rasmi kazi
ya Uwakilishi wa Heshima baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kidiplomasia.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.