Thursday, March 12, 2020

Balozi Amour katika juhudi za kutafuta fursa nchini Kuwait

Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhandisi Aisha S. Amour amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Fawaz Al-Khaled Al-Hamad Al-Sabah, Gavana wa Mkoa wa Ahmadi, Kuwait.  Uongozi huo wa Mkoa wa Ahmadi ulionyesha utayari wa kushirikiana na Mkoa mmojawapo wa Tanzania katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo mara baada ya kukubaliana kwa kupitia Wizara ya Mambo Nje ya Kuwait.

Mhe. Mhandisi Aisha S. Amour, Balozi wa Tanzania nchini Kuwait akipokea zawadi ya alama ya Mkoa toka kwa Mhe. Fawaz Al-Khaled Al-Hamad Al-Sabah, Gavana wa Mkoa wa Ahmadi, Kuwait katika ofisi za Mkoa huo, ambapo Mhe. Balozi alifanya ziara.

Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhandisi Aisha S. Amour atembelea ofisi za Mamlaka ya Kilimo na Uvuvi ya Kuwait na kufanya mazungumzo na Mhe.Mohamed Al-Yousef Al-Sabah, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo.  Mkurugenzi huyo alieleza utayari wa kushirikiana na Mamlaka za Tanzania katika sekta ya kilimo na uvuvi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika tafiti na teknolojia mbalimbali hasa katika mbegu, kilimo cha umwagiliaji, pamoja na kilimo cha kitalu nyumba.
 Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhandisi Aisha S. Amour atembelea mashamba ya tafiti wa kilimo cha mbogamboga kwa upandaji wa kawaida. Kushoto kwa Mhe. Balozi ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti wa mazao, Dr. Reem Ahmed Al-Hazeem.
Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhandisi Aisha S. Amour akiangalia uzalishaji wa bilinganya kwa ajili ya utafiti kwa kwa njia ya kitalu nyumba, ‘greenhouse.

Balozi wa Tanzania nchini Kuwait Mhandisi Aisha S. Amour akingalia uzalishaji wa matango kwa ajili ya utafiti kwa njia ya kitalu nyumba.
 Balozi wa Tanzania nchini Kuwait. Mhe. Mhandisi Aisha S. Amour alikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Balozi Abdulhamid Al-Failakawi, Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje ya Kuwait – Idara ya Afrika. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Eng. Aisha aliwasilisha salamu za shukrani kwa Serikali ya Kuwait kwa ushirikiano mkubwa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kupitia Kuwait Fund. Aidha, alieleza fursa mbalimbali za uwekezaji, biashara na Utalii zilizopo Tanzania na kumuomba kuwezesha katika kukutana na Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali ya Kuwait ili kuangalia uwezekano wa ushirikiano kati ya Kuwait na Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhe. Mhandisi Aisha S. Amour afanya mazungumzo na Bw. Emad Abdullah Al-Zaid, Mkurugenzi Msaidizi wa Kuwait Chamber of Commerce & Industry kuhusu kupanga mikakati ya kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Kuwait pamoja na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo Tanzania. 

Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhe. Mhandisi Aisha S. Amour atembelea kiwanda cha AlHomaizi Food kiwanda cha kuchakata nafaka.  Al-Homaizi ni Kampuni mama ya Alrifai ambayo imeanza kununua korosho za Tanzania na kuzisafirisha nchi za Mashariki ya kati ikiwa ni pamoja na Kuwait.

Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhandisi Aisha S. Amour akiwa katika maabara ya kiwanda hicho, akipewa maelezo namna ya upimaji ubora wa mazao ya nafaka kabla ya kuchakata na baada.

 Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhandisi Aisha S. Amour akutana na kufanya mazungumzo na Bw. Ahmad A. Eid, Mkurugenzi Mtendaji wa Ushirika wa Kuwait Shipping Companies & Agent Association kuhusu fursa za uwekezaji na usafirishaji wa baharini. Bw. Ahmad alieleza utayari wa kuleta meli nchini Tanzania kuchukua mizigo ya biashara moja kwa moja kutoka Tanzania mpaka Kuwait.
Balozi wa Tanzania nchini Kuwait. Mhandisi Aisha S. Amour,  akutana na kufanya mazungumzo viongozi wa Umoja wa Watalii Kuwait kuhusu masuala ya utalii Tanzania. Katika mazungumzo na viongozi hao ambao wanawanachama Zaidi ya 150, ilikubalika kuandaa kwa safari ya watalii Zaidi ya 70 kuja Tanzania mwezi Julai 2020. Aidha, viongozi hao walikubali kuwa mabalozi wa utalii wa Tanzania nchini Kuwait.
 Balozi wa Tanzania nchini Kuwait. Mhe. Mhandisi Aisha S. Amour akutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Automobile Agents kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania katika sekta hiyo. Viongozi hao walikubali kufikisha taarifa kwa wajumbe wa umoja wao na kujipanga kufika Tanzania kuangalia utaratibu wa uwekezaji katika sekta yao ya magari.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.