Mkutano wa
Maafisa Waandamizi ambao ni mkutano wa awali wa maandalizi ya Baraza la
Mawaziri la nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaotarajia
kufanyika tarehe 18 Machi 2020 umefunguliwa rasmi katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini
Dar es Salaam.
Akifungua
mkutano huu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafisa Waandamizi wa SADC, Balozi Kanali
Wilbert Ibuge amewashukuru wajumbe wote kutoka nchi wanachama pamoja na
wataalamu wa TEHAMA kwa jitihata walizoonesha kuhakikisha mkutano huu kwa mara
ya kwanza unafanyika kwa mfumo wa Video. “ Hii ni uthibitisho siyo tu wa namna
ambavyo Teknolojia ya Habari na Mawasilisno imebadilisha na itaendelea
kutubadilisha namna tunavyowasiliana bali pia ambavyo matishio ya majanga ya
kidunia kama ugonjwa wa Virusi vya CORONA (COVID 19) yanavyotulazimisha kutafuta
mbinu mbadala za kufanya mambo yetu kikanda na kidunia pamoja na kuendelea kuimarisha
ushirikiano bila kuonana ana kwa ana” alisema Balozi Ibuge
Mkutano huu unahudhuriwa na Maafisa Waandamizi
kutoka nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) wenye dhamana
ya masuala ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha, Uchumi, Mipango
pamoja na Viwanda na Biashara.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu unaongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharikia na Mwenyekiti wa Kamati ya
Maafisa Waandamizi wa SADC, Balozi Kanali Wilbert Ibuge ambaye ameambatana na
maafisa wengine waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Wizara ya Fedha na Mipango Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Wizara ya Viwanda na Biashara Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Maafisa wengine waandamizi walioshiriki ni pamoja na maafisa kutoka Wizara
ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mambo ya Ndani. Vilevile mkutano huu
umehudhuriwa na baadhi ya Mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha katika nchi za
SADC ambao ni pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Mkutano huu utajadili ajenda chache za muhimu kwa wakati huu ambazo ni:
Taarifa ya Maandalizi ya Dira ya SADC ya 2050; Mpango Mkakati wa Maendeleo wa
SADC 2020-2030; Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC tangu kuanzishwa kwake mwaka
1980; Utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita; Hali ya michango na kifedha
kwa ujumla ya SADC; na Kupokea taarifa ya ukaguzi wa shughuli mbalimbali za
Sekretarieti SADC.
Awali mkutano katika ngazi ya Maafisa Waandamizi ulipangwa kufanyika
kuanzia tarehe 12 hadi 14 Machi 2020 na kufuatiwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri
tarehe 17 na 18 Machi 2020. Hata hivyo, kufuatia ushauri na mapendekezo
yaliyotolewa na Mawaziri wa Afya kutoka Nchi Wanachama wa SADC walipokutana kwa
dharura tarehe 9 Machi, 2020. Mkutano huo ulijadili na kupendekeza kwa Nchi
Wanachama namna ya kuzuia maambukizi ya mlipuko wa ugonjwa hatari wa virusi vya
Corona (COVID 19) unaosambaa kwa kasi na kuleta athari kubwa duniani tangu
kubainika kwakwe mwezi Desemba.
===================================================================
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.