Friday, March 20, 2020

WIZARA YAKUTANA NA KAMATI YA BUNGE YAWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI KWA MWAKA 2019/2020


 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Wizara ya Mpango wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2019/2020 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika moja ya kumbi za Bunge jijini Dodoma.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Salim Mwinyi Rehani (mwenye suti nyeusi) wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi hayupo pichani aliyekuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Wizara ya mwaka 2019/2020


 WIZARA YAKUTANA NA KAMATI YA BUNGE YAWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI KWA MWAKA 2019/2020

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2019/2020.

Akiwasilisha taarifa ya Wizara, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi amesema Wizara katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuzingatia maoni na ushauri wa Kamati ya Bunge imeanzisha Kitengo cha Usimamizi wa Majengo ambacho kitakuwa chini ya Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu.

Amesema pamoja na kuanzishwa kwa Kitengo hicho Wizara imeendelea kushirikiana na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi huku wakifuata sheria na taratibu zilizopo.

Amesema uamuzi wa kuanzishwa kwa kitengo hicho unatokana na ushauri uliotolewa na Kamati hiyo uliyoitaka Wizara kuhakikisha mipango ya ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi ya Balozi mbalimbali nje ya nchi unasimamiwa kitaalamu na kwa ufanisi mkubwa.

“Uamuzi huu umetokana na ushauri ambao Kamati hii iliutoa kwa Wizara katika kuhakikisha suala la ujenzi wa majengo ya Balozi zetu unasimamiwa kitaalamu na kwa ufanisi,” alisema Prof. Kabudi.

Mhe. Waziri amesema Wizara inaendelea na mipango ya kuwashirikisha Watanzania waishio ughaibuni katika mipango na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchininikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira rafiki ya kuchangia maendeleo na kusaidia ndugu na jamaa zao waliopo nchini na kufanya uchambuzi wa mazingira ya ushirikishwaji wao na kuangalia masuala ya kisheria, kitaasisi ushirikiano na sekta binafsi takwimu za Watanzania waishio ughaibuni na uwezo na hamasa ya kuchangia maendeleo ya nchi.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.