Tuesday, March 3, 2020

PROF. KABUDI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA UN, UNHCR


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić Pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Antonio Canhandula Jijini Dar es Salaam.

Waziri Kabudi amewaeleza Bw. Milišić na Bw. Canhandula kuwa UN pamoja na UNHCR zimekuwa na mchango mkubwa kwa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza maendeleo pamoja na zile za kushughulikia masuala ya wakimbizi.

“Kwa ujumla UN imekuwa ikisaidia Tanzania kufanikisha agenda zake za maendeleo endelevu ya kijamii, na kiuchumi hivyo Serikali itaendelea kuhakikisha inaendeleza uhusiano huu," Amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wake Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa nchini (UN) Bw. Milisic amesema kuwa uhusiano wa UN na Serikali ya Tanzania ni wa muda mrefu na hivyo ni jukumu la UN kuhakikisha inaimarisha uhusiano huo na kuuboresha.

 “Ni matumaini yangu kuwa uhusiano huu tutauboresha vizuri na kuimarisha kwa maslahi mapana na maendeleo endelevu ya taifa la Tanzania," Amesema Bw. Milišić

Nae Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Canhandula amesema wanatambua mchango mkubwa ambao Tanzania imekuwa ikiutoa kuhakikisha inaimarisha ulinzi wa maeneo ya wakimbizi ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kuishi kwa amani na utulivu pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu kama vile malazi na mavazi.

"Kwa kweli UNHCR tunafurahishwa na jinsi Serikali ya Tanzania ambavyo imekuwa ikipokea wakimbizi na kuwapatia baadhi ya mahitaji muhimu……tunaomba tuendeleze ushirikiano huu kwa maendeleo yetu," Amesema Bw. Canhandula.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimfafanulia jambo Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiisoma hati ya utambulisho mara baada ya kuipokea kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Antonio Canhandula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kabla ya kukabidhi hati ya utambulisho katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea hati ya utambulisho kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Antonio Canhandula katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.