Tuesday, March 17, 2020

DKT. NDUMBARO AKUTANA NA BALOZI WA UBELGIJI, SWEDEN


Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ubelgiji nchini, Mhe. Peter Van Acker pamoja na Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjoberg leo jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo ya Mhe. Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro pamoja na Balozi wa Ubelgiji yalijikita katika masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ubelgiji hasa kwenye sekta za Kilimo na Madini.

Balozi wa Ubelgiji, Mhe. Acker amesema kuwa Ubelgiji itaendelea kuwekeza katika kilimo cha maharage mkoani Kigoma, na kilimo cha Tumbako katika mikoa ya Tabora, Ruvuma, Katavi na Rukwa.

"kupitia uwekezaji wa kilimo nchi zetu mbili (Tanzania na Ubelgiji) zimekuwa zikinufaika sawa hivyo ni rai yangu kuona uwekezaji huu unaendelea kutoa fursa za ajira kwa mataifa haya mawili," Amesema Balozi Acker.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa Tanzania itaendelea kuhakikisha inazidi kuimarisha Uhusiano wake na Ubelgiji katika sekta ya Kilimo, Uwekezaji na Biashara ili kuendelea kutoa fursa za ajira na kukuza uwekezaji nchini.

Katika nyingine, Naibu Waziri Dkt. Ndumbaro amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjoberg, ambapo mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.  

Pamoja na mambo mengine, Balozi wa Sweeden nchini Mhe. Sjoberg amemuahidi Naibu Waziri kuwa Sweeden itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa nchi hizi mbili zinapiga hatua katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kwa upande wake Mhe. Naibu Waziri amemhakikishia Balozi Sjoberg kwamba Tanzania itaendelea kukuza na kuimarisha Ushirikiano na Uhusiano wake na Sweden kwani uhusiano huo wa muda mrefu umekuwa na manufaa kwa nchi zote mbili.


Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akisalimiana na Balozi wa Ubelgiji nchini, Mhe. Peter Van Acker kabla ya kuanza kwa mazungumzo yao jijini Dar es Salaam



Balozi wa Ubelgiji nchini, Mhe. Peter Van Acker akiongea na Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam



Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akimfafanulia jambo Balozi wa Ubelgiji nchini, Mhe. Peter Van Acker wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam



Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Balozi wa Sweeden nchini Mhe. Anders Sjoberg wakisalimiana bila kushikana mikono kabla ya kuanza kwa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam



Balozi wa Sweeden nchini Mhe. Anders Sjoberg akiongea na Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam



Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akimueleza jambo Balozi wa Sweeden nchini Mhe. Anders Sjoberg wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.