Mhe. Prof. Kabudi akiagana na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nje, Ulinzi na Usalama mara baada ya kukamilisha ziara yao kwenye Jengo la Wizara lililopo Mtumba jijini Dodoma ====================================================
WAJUMBE WA KAMATI YA BUNGE YA NJE, ULINZI NA USALAMA WATEMBELEA JENGO LA WIZARA LILILOPO MTUMBA
Wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU)
wakiongozwa na Mhe. Victor Mwambalaswa (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati hiyo
wamefanya ziara ya kikazi kwenye Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki lililopo kwenye Mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma leo
tarehe 15 Machi 2020.
Wajumbe
hao ambao wapo kwenye program ya kukagua miradi iliyopo kwenye Wizara
zinazosimamiwa na Kamati hiyo, wamepokelewa na mwenyeji wao Mhe. Prof.
Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki mara baada ya kuwasili.
Wakizungumza
wakati wa ziara hiyo, baadhi ya Wajumbe hao, wameipongeza Wizara kwa kukamilisha ujenzi
wa jengo hilo kwa wakati ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya
Tano ya kuhamia Dodoma. Pia wameishauri Wizara kuendelea kuboresha maeneo
kadhaa katika jengo hilo ikiwa ni pamoja na kuweka uzio kuzunguka jengo hilo na
kukamilisha mfumo wa TEHAMA kwa ajili ya kuboresha mawasiliano. Vilevile,
Wajumbe wa Kamati hiyo wameitaka Wizara kuzingatia kanuni za ujenzi wa majengo
ya Ofisi za Mambo ya Nje pale Wizara itakapoanza ujenzi wa jengo lake la kudumu
katika siku zijazo.
Kwa
upande wake, Mhe. Prof. Kabudi aliahidi kutekeleza ushauri uliotolewa na
Wajumbe wa Kamati hiyo na kuwahakikishia kuwa, mapungufu kadhaa yaliyopo
yatafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
Aidha,
akitoa taarifa fupi kuhusu ugonjwa wa Corona kwa Wajumbe wa Kamati hiyo, Mhe.
Prof. Kabudi alisema kuwa, Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti kwa
ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo endapo utaingia nchini. Hatua hizo ni
pamoja na mikutano ya kikanda kuanza kufanyika kwa njia ya video ukiwemo
Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
utakaofanyika nchini kuanzia tarehe 16 hadi 18 Machi 2020.
Pia
Kamati ya Kitaifa inayojumuisha Sekta mbalimbali imeundwa kwa ajili ya kuandaa
mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ugonjwa huo. Kadhalika vifaa, wataalam na
maeneo ya karantini tayari yametengwa kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.
“Tanzania
inaendelea kuchukua tahadhari mbalimbali kuhusu ugonjwa wa Corona ambao hadi
sasa haujaingia nchini. Hatua hizo ni pamoja na kuandaa mikutano ya kikanda
ambayo itafanyika kwa njia ya video. Katika kutekeleza hilo, Mkutano wa Baraza
la Mawaziri wa SADC unaoanza tarehe 16 Machi mwaka huu utafanyika kwa njia ya
video na utafuata taratibu zote za mikutano ya kikanda wakati wa ufunguzi”
alisisitiza Prof. Kabudi.
Jengo
la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambalo lipo Mtumba
jijini Dodoma lina ukubwa wa Mita za Mraba 1,002 na vyumba 17 vyenye matumizi
mbalimbali zikiwemo Ofisi. Jengo hilo lilianza kujengwa mwezi Desemba 2018 na kukamilika
mwezi Machi 2019.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.