KATIBU MKUU BALOZI KANALI IBUGE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA NCHINI KWA NJIA YA VIDEO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akiwa Dodoma, terehe 30 Machi 2020 amefanya mazungumzo kwa njia ya video (video conference) na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke.
Pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya mahusiano ya pande mbili (bilateral relations), viongozi hawa walizungumzia utayari wa Serikali wa nchi zote mbili katika kupambana na mgonjwa wa COVID-19. Sambamba na utayari huo, Katibu Mkuu alimfahamisha Balozi Wang Ke kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya corona. Wakati huohuo, alimweleza kuhusu utayari wa Serikali kushirikiana na wadau wengine duniani ikiwemo China katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona.
Vilevile, Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, kwa jitihada kubwa walizozifanya kiasi cha kufanikiwa kudhibiti kuenea zaidi kwa COVID-19 nchini humo na jitihada wanazozifanya ikiwemo kusaidia wataalamu, vifaa tiba na vya kujikinga kwa Mataifa mengine duniani ambapo COVID-19 inaendelea kuleta madhara. Hadi sasa China imefanya mazungumzo na nchi 24 za Afrika ikiwemo Tanzania yanayolenga kushauri na kubadlishana uzoefu na taarifa muhimu zitakazo saidia kutokomeza COVID-19.
Aidha,katika mazungumzo hayo Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke amebainisha kuridhishwa kwake juu ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona. Balozi Wang Ke aliongezea kusema pamoja na kutokuwepo maambukizi mapya nchini China, Serikali ya nchi hiyo bado inaendelea kuchukua tahadhari na hatua za kuzuia maambukizi mapya, na kuwa wataendelea kutoa mchango kwa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na COVID-19. Balozi Wang Ke amesisitiza kuwa, Serikali ya China ipotayari kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya COVID-19.
Katibu Mkuu ameushukuru Ubalozi wa China kwa utayari wake wa kushirikiana na Tanzania dhidi ya mapambano ya COVID-19, na kueleza kwamba Wizara itawasiliana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ili kuandaa orodha ya mahitaji ambayo Ubalozi wa China unaweza kusaidia. Katibu Mkuu alirejea kauli ya Serikali kwamba mapambano dhidi ya virusi vya corona ni vita ambayo Tanzania haina budi kukabiliana navyo, kwa ujumla wake na kwamba hatua zote ambazo Tanzania inachukua chini ya uongozi wa Waziri Mkuu zinalenga kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo bila kuathiri shughuli za kila siku. Alisistiza kwamba Tanzania inaamini kwa jitihada inazochukua na kwa ushirikiano kutoka China itafanikiwa kushinda janga hili.
Mwisho, Balozi Wang Ke alimpongeza Katibu Mkuu kwa kuendelea kufanya mikutano na Waheshimiwa Mabalozi licha ya changamoto iliyopo ya COVID-19 kwa kuweka utaratibu wa kufanya kwa mikutano hiyo kwa njia ya Video akiwa Ofisini kwake Mtumba, Dodoma wakati Mabalozi wakiwa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.