Ubalozi wa Tanzania nchini India wakishirikiana na Shirika
la Ndege la Tanzania [Air Tanzania] waliandaa Kongamano la Biashara na
Uwekezaji lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Mumbai
ambapo wafanyabiashara wapatao 40 kutoka Tanzania, Maofisa kutoka Kituo Cha
Uwekezaji [Tanzania Investment Centre] na “Air Tanzania” walikutanishwa na wafanyabiashara,
wawekezaji na wasafirishaji wa bidhaa wa India wapatao 60.
Pamoja na mambo mengine kongamano hilo lililenga kuwakutanisha
wafanyabiashara, wawekezaji na
wasafirishaji wa bidhaa wa Tanzania na India ili kupanua wigo wa biashara
kati ya Tanzania na India hususan, ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa Tanzania
kuja India. Wafanyabiashara wa Tanzania walipata fursa adhimu ya kubadilishana
taarifa zinazohusu bidhaa zinazozalishwa kwa wingi Tanzania kwa minajili ya
kupata masoko zaidi ya bidhaa hizo na
kuongeza idadi ya mizigo inayosafirishwa na ‘Air Tanzania’ kutoka Dar es Salaam kuja Mumbai.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Balozi wa
Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alieleza, pamoja na mambo mengine,
kuwa Kongamano hilo litasaidia wafanyabiashara wa
Tanzania kukutana na wenzao wa India na kuanzisha uhusiano wa kibiashara
unaotarajiwa kufungua masoko zaidi ya bidhaa zao nchini baada ya wadau hao
kupata maelezo ya kutosha kuhusu bidhaa wanazozalisha nchini na faida zake.
Kwa ujumla, India ina soko kubwa la bidhaa. Hivyo,matarajio
ni kuona kiwango cha bidhaa kutoka
Tanzania zinazouzwa India kinaongezeka zaidi hususan, baada ya kurejeshwa tena
kwa ndege za Shirika la Ndege, Tanzania, kati ya Dar es Salaam na Mumbai mwezi
Julai 2019. Balozi Luvanda alitoa rai
kwa wafanyabiashara hao kutumia usafiri wa ‘Air Tanzania’ kwa kuwa ni wa
uhakika, wa muda mfupi zaidi na pia bei yake ni nafuu. Aidha, Mhe. Luvanda aliwaomba wafanyabiashara hao kuongeza
ushirikiano na Tanzania katika utalii, hasa ikizingatiwa kuwa India inatoa
watalii zaidi ya milioni 20 kwa mwaka kutembelea nchi mbalimbali duniani.
Akimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania,
Bwana Patrick Ndekana alieleza historia ya Shirika hilo na hali ilivyo kwa
sasa. Aidha, Bwana Ndekana aliwaeleza washiriki wa Kongamano kuwa Shirika hilo
limejipanga kuhakikisha usafiri wa uhakika, bora na salama kwa kuwa linamiliki
ndege mpya na za kisasa.
Vilevile, Bwana Ndekana alifafanua shabaha ya kuitisha
Kongamano kuwa ilitokana na wadau mbalimbali kama vile wasafairishaji wa bidhaa
kukosa taarifa za fursa za usafirishaji zilizopo kwenye shirika hilo. Hivyo,
alieleza matarajio ni kuwa wadau hao wataweza kutumia zaidi usafiri wa Shirika
hilo baada ya Kongamano hilo mahsusi.
Akiwasilisha mada kuhusu biashara na uwekezaji nchini
Tanzania, Afisa kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania [TIC], Bwana Nestory
Kissima alieleza kuwa Tanzania imefanya mabadiliko makubwa katika sera zake za
kuvutia biashara na uwekezaji na amewaomba wafanyabiashara waliohudhuria
kongamano hilo kuchangamkia fursa za biashara zilizopo Tanzania hususan, katika
ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya asili ya biashara kama vile mkonge,
pamba, korosho,madini,matunda mbalimbali kama vile parachichi, na nafaka
mbalimbali pamoja na ununuzi wa mazao hayo ambayo yanahitajika sana nchini
India.
Bwana Kissima alieleza kuwa, kwa kiasi
kikubwa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini Tanzania
yameboreshwa ikiwa ni pamoja na Serikali kufanyia kazi changamoto mbalimbali
zilizokuwepo kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Jitihada hizo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwenye viwanda na miradi
ya kimkakati ifikapo 2025.inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya
uchumi wa kati kupitia uwekezaji
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akihutubia wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Mumbai tarehe 05 Machi 2020. |
Kaimu Mkurugenzi wa Air
Tanzania akizungumza katika
Kongamano hilo.
|
Bwana Nestory Kissima, kutoka Kituo cha Uwekezaji
Tanzania [TIC ] akiwasilisha mada katika Kongamano hilo.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.