Wednesday, March 4, 2020

DKT. NDUMBARO AKUTANA,KUFANYA MAZUNGUMZO NA MASENETA KUTOKA UFARANSA


Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Maseneta sita (6) kutoka Ufaransa walioko kwenye ziara nchini.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam ambapo ujumbe wa Maseneta hao unaongozwa na Mhe. Hervé Maurey, Mwenyekiti wao ambae pia ni Rais wa Kamati ya Bunge ya Mipango Miji na Maendeleo Endelevu pamoja na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Frederic Clavier.

Katika mazungumzo hayo ujumbe wa maseneta umeeleza kuridhishwa na jitihada mbalimbali za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi kupitia uwekezaji kwenye miundombinu na kutunza mazingira.

Kwa upande wake Naibu Waziri Dkt. Ndumbaro ametumia fursa hiyo kuueleza ujumbe huo sekta ambazo Tanzania inaweza kushirikiana na Ufaransa ili kukuza zaidi ushirikiano baina ya nchi hizi mbili uliodumu kwa muda mrefu.

Ametaja sekta hizo kuwa ni pamoja na sekta ya kilimo na mifugo, madini, utafiti katika vyuo vikuu pamoja na utalii na utunzaji wa mazingira.

"Katika kipindi hiki Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeweka kipaumbele kuendeleza viwanda hususan viwanda vya kuongeza thamani, amesema Dkt. Ndumbaro.

Naibu Waziri aliongeza kuwa, "Tanzania ina mazingira bora ya uwekezaji na niwasihi tu mtufikishie taarifa hizi kwa wawekezaji wanaoweza kuja kuwekeza nchini katika viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na kiwanda cha kuunganisha magari," Amesema Dkt. Ndumbaro. 


Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiongea na Ujumbe wa Maseneta sita (6) kutoka Ufaransa leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Mwenyekiti wa Ujumbe wa Maseneta kutoka Ufaransa, Bw. Herve Maurey (upande wa kulia mwa Naibu Waziri) akifafanua jambo wakati wa maongezi baina yao na Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Mwenyekiti wa Maseneta kutoka Ufaransa, Bw. Herve Maurey akimkabidhi zawadi Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro



Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Maseneta kutoka Ufaransa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.