Wednesday, May 31, 2023

MAKAMU WA RAIS DKT MPANGO AMWAKILISHA MHE. RAIS SAMIA MKUTANO MAALUM WA WAKUU WA NCHI WA EAC JIJINI BUJUMBURA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Dharura wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao umefanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 31 Mei 2023.

 

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mikutano ya Kamati ya Uratibu ya Makatibu Wakuu na Mkutano Maalum wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya  hiyo, pamoja na mambo mengine umejadili hali ya Usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo viongozi hao wameeleza kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na Jumuiya katika kutafuta amani ya kudumu katika eneo hilo.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Burundi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Evariste Ndayishimiye amesema kuwa anawapongeza Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kuhakikisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inaedelea kustawi kwa maslahi mapana ya wananchi wa nchi  zao.

 

Amesema mara zote, Wakuu hao wa Nchi wameonesha utayari wa kutafuta suluhu ya haraka kwa changamoto za Jumuiya hiyo ikiwemo kushirikiana kwa pamoja katika kutafuta amani ya kudumu katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

 

“Nawapongeza viongozi wenzangu kwa utayari wenu wa siku zote katika kutafuta changamoto mbalimbali zinazoikabili Jumuiya yetu ikiwemo kutafuta  amani ya kudumu  katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Pia navipongeza vikosi vya Kanda vya Jumuiya ya Afrika Mashariki vilivyopo Congo kwa kuendelea kulinda amani katika eneo hilo la Mashariki mwa Congo” alisema Mhe. Rais Ndayishimiye.

 

Kadhalika Mkutano huo umemteua Jaji wa Makakama ya Rufaa ya Tanzania, Mhe. Omar Othman Makungu kuwa Jaji wa Kitengo cha Rufaa katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki. Mhe. Makungu anachukua nafasi ya Mhe. Jaji Sauda Mjasiri  kutoka Tanzania ambaye amestaafu.

 

Vilevile, Wakuu hao wa nchi wamemteua na kumwapisha Jaji Kayembe Kasanda Ignace Rene kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa Jaji wa Mahakama ya Divisheni ya Awali ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.

 

Kadhalika Mkutano huo umeteua na kuwaapisha  Naibu Makatibu Wakuu wawili ambao ni Bi. Annette Ssemuwemba Mutaawe kutoka Jamhuri ya Uganda kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umoja wa Forodha, Biashara na Masuala ya Umoja wa Fedha na Bw. Andrea Aguer Ariik Malueth kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Miundombinu, Sekta za Uzalishaji, Kijamii na Siasa.

 

Bi. Annette anachukua nafasi ya Mhandisi Steven Mlote kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye mkataba wake wa kazi umemalizika na Bw. Malueth anachukua nafasi ya Mhe. Christopher Bazivamo kutoka Rwanda ambaye naye mkataba wake umefikia ukomo.

                                                       

Mbali na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango mkutano huo pia umehudhuriwa na Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto pamoja na Wawakilishi wa Marais wa Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,   Uganda na Sudan Kusini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Mpango akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano Maalum wa  21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 31 Mei 2023. Wengine katika picha ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi
Mhe. Dkt. Mpango pamoja na ujumbe aliiongozana nao wakishiriki Mkutano Maalum wa  21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 31 Mei 2023.
Mkutano Maalum wa  21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea jijini Bujumbura, Burundi tarehe 31 Mei 2023.

Mhe. Waziri Bashungwa na Balozi Mbundi wakati wa mkutano
Picha ya pamoja




 

WAZIRI TAX AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA URUSI NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Shirikisho la Urusi nchini, Mhe. Andrey Avetisyan katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma Leo tarehe 31Mei 2023.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Urusi pamoja na sekta za ushirikiano zilizo katika hatua mbalimbali kwa maslahi ya pande zote mbili.

Vilevile, katika mazungumzo hayo wamejadili juu ya mkutano wa Urusi – Afrika na Kongamano la Uchumi litakalofanyika mwezi Julai 2023 nchini Urusi. Kongamano hilo linatarajiwa kutoa mtazamo wa uhusiano kati ya Urusi na na nchi za Afrika.

Tanzania na Urusi zinashirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi, afya, biashara, viwanda, uwekezaji na utalii ambapo kwa pamoja zimekubaliana kuendeleza ushirikiano huo ili kuleta tija katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana Balozi wa Shirikisho la Urusi nchini, Mhe. Andrey Avetisyan baada ya kuwasili katika ofisi za Wizara jijini Dodoma kwa mazungumzo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kulia) katika picha ya pamoja na Balozi wa Shirikisho la Urusi nchini, Mhe. Andrey Avetisyan baada ya kuwasili katika ofisi za Wizara jijini Dodoma kwa mazungumzo


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kulia) akimsindikiza na Balozi wa Shirikisho la Urusi nchini, Mhe. Andrey Avetisyan baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika katika ofisi za Wizara jijini Dodoma kwa mazungumzo


Tuesday, May 30, 2023

BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akiwasilisha makadirio ya Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 bungeni Dodoma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akijibu hoja zilizowasilishwa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 bungeni Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kushoto) pamoja na Naibu Katibu MKuu wa Wizara hiyo Mhe. Balozi Fatma Rajab wakifuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara  kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 bungeni Dodoma

Sehemu ya uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na baadhi ya mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa nchini wakifuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara  kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 bungeni Dodoma 

Bunge likiendelea 




 

Monday, May 29, 2023

MKUTANO MAALUM WA MAWAZIRI WA ULINZI WA EAC WAFANYIKA JIJINI BUJUMBURA

Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujadili hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umefanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 29 Mei 2023.

 

Akifungua Mkutano huo, Waziri wa Ulinzi wa Burundi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Alain Tribert Mutabaze, amesema jitihada za pamoja ikiwemo mikakati mipya ya namna ya kukabiliana na vikundi vya waasi katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado zinahitajika ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika eneo hilo.

 

Amesema  pamoja na kupongeza jitihada nyingi zinazofanywa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki  ikiwemo kupeleka Kikosi cha Kulinda amani cha Jumuiya (EACRF),  bado ipo haja ya kufanya tathmini ya mara kwa mara ya mikakati iliyopo kama inaleta tija na kuandaa mikakati  mipya ikiwa ni pamoja na kuviwezesha Vikosi hivyo  ili viweze kutekeleza kikamilifu jukumu la  kulinda amani  katika eneo hilo.

 

“Changamoto katika eneo la Mashariki mwa Congo bado zipo. Tunatakiwa kuboresha mikakati yetu na kufanya tathmini za mara kwa mara ya maendeleo ya jitihada hizi,  kwani hali inayoendelea Mashariki mwa Congo inatuathiri sote kama jumuiya kwa namna moja au nyingine. Hivyo niwaombe Waheshimiwa Mawaziri tuje na mapendekezo yenye tija  tutakayoyawasilisha kwa Wakuu wetu wa Nchi kwa mustakabali wa eneo  hilo la Mashariki mwa Congo na sisi sote” amesema Mhe.  Mutabaze.

 

Mhe. Mutabaze pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Mawaziri hao nchini Burundi na kuwaomba kutumia muda wao kujadili na kuandaa mapendekezo yatakayoleta suluhu ya kudumu nchini DRC hususan eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.

 

Awali akizungumza kwenye mkutano huo,  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,  Dkt. Peter Mathuki amesema  Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Nchi Wanachama ili kuhakikisha amani na utulivu wa kudumu unapatikana katika eneo la Mashariki mwa Congo.

 

Mkutano huo umewahusisha Mawaziri wa Ulinzi kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Makatibu Wakuu  na Wakuu wa Majeshi.

 

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb.) na kumshirikisha pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,  Dkt. Faraji Mnyepe, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko, Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi pamoja na Maafisa wengine waandamizi kutoka Serikalini.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa (kulia) ambaye pia anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo   akizungumza wakati wa mkutano huo uliofanyika Bujumbura, Burundi tarehe 29 Mei 2023. Wengine katika picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko.
Waziri wa Ulinzi wa Burundi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Masahriki, Mhe. Alain Tribert Mutabaze akifungua rasmi Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo uliofanyika jijini Bujumbura tarehe 29 Mei 2023
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki akizungumza wakati wa Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 29 Mei 2023
Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi (kulia) akishiriki Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 29 Mei 2023
Ujumbe wa Burundi katika Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Ujumbe wa Sudan Kusini ukishiriki Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Ujumbe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Ujumbe wa Kenya ukishiriki Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Mhe. Bashungwa kwa pamoja na Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe na Mhe. Balozi Maleko wakiimba wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
.
Sehemu ya Ujumbe wa Rwanda ukishiriki wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Balozi Mbundi na washiriki wengine wakiimba wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Mnyepe akiteta jambo na Balozi Maleko kabla ya kuanza kwa Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo


ehemu ya ujumbe wa Tanzania wakishiriki Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania wakishiriki Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Picha ya pamoja

Picha ya pamoja