Thursday, May 18, 2023

MAMBO YA NJE YAAINISHA FURSA ZINAZOPATIKANA KATIKA MIKUTANO YA KIMATAIFA

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akijibu swali bungeni jijini Dodoma lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Neema Kichiki Lugangira tarehe 18 Mei 2023. 
=================================


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amefafanua fursa mbalimbali zinazopatikana nchini kupitia ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya kimataifa.

Ufafanuzi huo umetolewa Bungeni jijini Dodoma leo tarehe 18 Mei 2023 wakati Mhe. Balozi Mbarouk akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Neema Kichiki Lugangira aliyetaka kujua ni kwa kiasi gani ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya Kimataifa unazingatia upatikanaji wa fursa za kiuchumi na utekelezaji wake.

Mhe. Balozi Mabarouk amesema kuwa, ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya Kimataifa unalenga kupata na kutumia fursa za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kupata mitaji, uwekezaji, masoko ya bidhaa na huduma, kukuza utalii, miradi ya kisekta, mikopo ya masharti nafuu na misaada, kujengewa uwezo wa kitaalamu, na upatikanaji wa teknolojia.

Mafanikio mengine ni pamoja na kupata masoko ya bidhaa mbalimbali kama vile mbogamboga, matunda, korosho, nafaka, nguo na mavazi, utalii, malumalu, na bidhaa za kioo. Vilevile, nchi yetu inanufaika kwa kupata wawekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utalii, viwanda, kilimo, uvuvi, mifugo, madini, na nishati jadidifu. 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.