Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameungana na waombelezaji mbalimbali kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 2007 hadi 2015, Ndugu Bernard Kamilius Membe katika viwanja kwa Karimjee jijini Dar Es Salaam tarehe 14 Mei, 2023.
Akitoa salamu za rambirambi, Mhe. Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa kuondoka kwa Ndugu Membe kumeleta masikitiko kwake binafsi, familia yake, Serikali, wadau mbalimbali, familia ya marehemu, wana Lindi na wananchi kwa ujumla.
“Msiba huu umewagusa watu wengi ndani na nje ya nchi, kutokana na uhodari wake katika masuala ya siasa na diplomasia, hivyo nguzo kuu imeondoka Mwenyezi Mungu awape wanafamilia subira katika kipindi hiki cha majonzi”
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ambaye pia ni mwenyeji wa tukio hilo la kuaga mwili, katika salamu zake za pole alieleza kuwa Wizara imempoteza kiongozi mahiri na hodari ambaye alijenga misingi mizuri katika kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.
“Marehemu Membe pamoja na kusimamaia maslahi ya nchi alitumia umahiri wake kuwajenga watumishi wa Wizara ambao kwa sasa wengine wanahudumu katika nafasi za Balozi”.
Aidha, Ndugu Membe alikuwa mcheshi, mwenye upendo na hodari hivyo Wizara itaendelea kuyaenzi mafanikio yaliyofanywa naye wakati wa utumishi wake.
Tukio hilo la kuaga mwili wa Marehemu Bernard Membe lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ambao ni pamoja na: Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa; Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma; Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu; Mawaziri, Manaibu Waziri, Wakuu wa Taasisi na Viongozi wengine wa Serikali, Taasisi binafsi na za dini na vyama vya siasa.
Wengine waliotoa salamu za rambirambi ni pamoja na: Mwakilishi wa kundi la wake wa Viongozi (Millenium group) Bi. Arafa Kikwete; Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe; Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Daniel Chongolo; Mkuu wa Mabalozi na Balozi wa Comoro nchini Tanzania, Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih; Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Amos Makala; Mtendaji Mkuu wa Mahakama (kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania), Prof. Elisante Ole Gabriel; na Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu.
=============================================
Pichani, sehemu ya Waombolezaji walioshiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,, Marehemu Bernard Membe. |
Gari lililobeba mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe likiwasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.