Mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe umewasili kijijini kwake Rondo mkoani Lindi kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho tarehe 16 Mei, 2023.
Mwili wa Marehemu Membe umewasili kijijini hapo majira ya saa 06.40 mchana na Helikopta ya Jeshi na kupokelewa na mamia ya waombolezaji kutoka sehemu mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Limdi, Mhe. Shaibu Ndemanga
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb.) aliongoza ujumbe uliosafiri na mwili wa marehemu Membe kutoka Jijini Dar es Salaam hadi Rondo mkoani Lindi. Mhe. Nape ni Mbunge wa Jimbo la Mtama ambalo awali liliongozwa na Marehemu Membe kwa miaka 15 mfululizo (2000-2015).
Mwili marehemu mara baada ya kuwasili nyumbani kwake ulipokelewa na wanafamilia kwa simanzi, huzuni pamoja na vilio.
Mwili huo utalala nyumbani kwake hadi kesho tarehe 16 Mei 2023 atakapopumzishwa katika nyumba yake ya milele.
Marehemu Membe aliaga Dunia tarehe 12 Mei, 2023 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kairuki, Jijini Dar es Salaam.
Helikopta ya Jeshi iliyobeba mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Marehemu Bernard Membe ikiwasili kijijini kwake Rondo |
Mwili wa Marehemu Bernard Membe ukiwa umebebwa na wananchi ulipowasili kijijini kwake Rondo |
Wananchi wa Rondo na kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwa wamejipanga kupokea mwili wa Marehemu Bernard Membe ulipowasili nyumbani kwake kijiji cha Rondo, Lindi. |
Sehemu ya waombolezaji wakiwa katika hali ya huzuni na majonzi kwenye msiba wa Marehemu Bernard Membe kijijini kwake Rondo, Lindi |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.