Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ametoa wito kwa Taasisi
mbalimbali nchini kuendelea kutunza kumbukumbu za historia ya Tanzania na
mchango wake katika medani za kikanda na kimataifa ili kuvirithisha vizazi vya
sasa na vijavyo.
Kauli hiyo ameitoa jijini
Dodoma tarehe 16 Mei 2023 wakati wa hafla fupi ya kikabidhi Machapisho ya
Hashim Mbita kwa Taasisi 18 zikiwemo za elimu.
Mhe. Dkt. Tax amesema
kuwa, Tanzania ina historia kubwa na nzuri katika medani za kikanda na
kimataifa ikiwemo mchango wake katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika
hivyo ni jukumu la wadau mbalimbali kuunganisha nguvu ya kutunza kumbukumbu ya
historia hiyo nzuri na kuvirithisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Ameeleza kuwa, Wizara
imeamua kuyakabidhi machapisho hayo kwa Taasisi hizo ili yasaidie kurithisha
historia iliyomo kwa vizazi vijavyo, na kujenga hamasa ya uzalendo kwa vizazi
vya sasa na vijavyo.
“Wizara inawakabidhi
nyinyi machapisho haya kama wawakilishi wa wengi. Tunaamini kupitia Vyuo na
Taasisi zenu machapisho haya yatawafikia na kusomwa na Watanzania wengi.
Vilevile kupitia machapisho haya historia kuhusu mchango uliotolewa na Tanzania
katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na Afrika kwa ujumla itatunzwa
na kukumbukwa daima” amesisitiza Mhe. Dkt. Tax.
Pia ameziomba taasisi hizo
kuwa chachu katika kueneza historia adhimu iliyomo kwenye chapisho hilo kwa
kuhakikisha linasomwa. “Pamoja na kulitumia chapisho hili kama rejea, na kuhamasisha
lisomwe, niwaombe wadau mbalimbali nchini kuona uwezekano wa kuandaa simulizi
au filamu ya chapisho ili kuweza kuwafikia watu wengi hususan vijana”
alisisitiza Mhe. Dkt. Tax.
Aidha, amefafanua kuwa, Chapisho
hilo ambalo pamoja na mambo mengine linaeleza harakati za ukombozi katika nchi
za Angola, Namibia, Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Msumbiji na mchango wan chi za
Tanzania, Zambia, Botswana, Lesotho, Malawi na Swaziland, lilipewa jina la
Hashim Mbita kutoka na mchango thabiti na uongozi mahiri wa Hayati Brigedia
Generali Hashim Mbita alioutoa akiwa
Katibu Mtendaji wa Kamati ya Kupigania Uhuru Afrika kuanzia mwaka 1972 hadi
1994.
Mhe. Dkt. Tax pia
ameshukuru na kupongeza mchango uliotolewa
na Viongozi mbalimbali wa Tanzania akiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Kamabarage Nyerere kwenye harakati za ukombozi kusini mwa Afrika kwani fikra na
mtazamo wake kuhusu umuhimu wa uhuru kwa nchi za Afrika zilifanikisha nchi zote
za Afrika kujikomboa dhidi ya ukoloni.
Pia Mhe. Dkt. Tax alitumia
fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya Kitanzania ya Uchapishaji ya Mkuki na Nyota kwa
kuchapisha chapisho hilo kwa umahiri.
“Nawashukuru wadau wote
waliofanikisha uchapishaji wa Chapisho la Hashim Mbita ikiwemo Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa
kuandaa Chapisho hilo lenye Volume 9 na kwa kutambua mchango wa Tanzania
katika harakati za Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Pia kipekee namshukuru Rais Mstaafu wa wa Awamu ya Nne wa
Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa kwa kuniagiza nikiwa Katibu Mtendaji wa
SADC na kunisisitiza kuhakikisha chapisho hili linakamilika baada mchakato wa
awali kusimama ambapo mwaka 2014 kufuatia maagizo hayo, mchakato ulitekelezwa
katika awamu tatu na kukamilika mwaka
2020” alifafanua Dkt. Tax.
Awali akimkaribisha Mhe.
Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amesema kwamba, Wizara imepokea
makasha 28 ya Chapisho la Hashim Mbita lenye Volume 9.
Pia aliongeza kusema
Sektretarieti ya SADC inaendelea na mchakato wa kutafsiri Chapisho la Hashim
Mbita kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kulisoma na
kuijua historia ya nchi yao hususan mchango wa Tanznaia katika Harakati za
Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Hafa hiyo ilihudhuriwa na
viongozi na wawakilishi kutoka Taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Rais,
Bunge, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Maktaba ya Taifa, Chuo Kikuu cha
Dodoma na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Sehemu ya wageni waalikwa walioshiriki hafla hiyo wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama |
Sehemu nyingine ya washiriki |
Mhe. Dkt. Tax akimkabidhi Bw. Mbwana Msingwa kutoka Ofisi ya Rais Kasha lenye Volume 9 za Machapisho ya Hashim Mbita |
Makabidhiano yakiendelea kwa wawakilishi wa taasisi mbalimbali ikiwemo Maktaba ya Taifa. |
Makabidhiano ya Machapisho ya Hashim Mbita yakiendelea |
Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) naye akikabidhiwa amachapisho ya Hashim Mbita |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.