Monday, May 22, 2023

KUKUA KWA KISWAHILI DUNIANI NI FURSA KWA TANZANIA

Wizara imelieleza Bunge kuwa imekuwa ikizitumia Ofisi za Balozi zilizoenea duniani kukuza Kiswahili na kuchangia ongezeko la fursa za ajira kwa Watanzania.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo tarehe 22 Aprili 2023 wakati wa kujibu swali la Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mhe.  Ameir Abdallah Ameir aliyetaka kujua namna Balozi zinavyotumia fursa ya kukua kwa Kiswahili duniani kutafuta ajira kwa Watanzania.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geofrey Pinda kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema kuwa Ofisi za Balozi zimeanzisha programu za kufundisha, kutafsiri na kufanya ukalimani wa Kiswahili duniani, hatua ambayo inatoa ajira kwa watanzania. Jumla ya balozi 13 zimeanzisha madarasa, vituo na club za Kiswahili. Kupitia programu hizo, zaidi ya watanzania 95 wamepata ajira katika maeneo hayo.

Vilevile, vyuo na vituo binafsi zaidi ya 150 vinafundisha Kiswahili duniani. Kwa sasa, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limepewa kazi ya kufundisha walimu kumi (10) wa Diaspora katika Ubalozi wetu wa Abu Dhabi ambao ulihitaji walimu wa kwenda kufundisha Kiswahili katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mhe. Naibu Waziri aliendelea kueleza kuwa Ofisi za Balozi zipo katika mazungumzo na vyuo vikuu kwenye maeneo yao ya uwakilishi ili Lugha ya Kiswahili iweze kujumuishwa katika mitaala ya vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kupata wahadhiri wa Kiswahili kutoka Tanzania.  Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kuwait, Chuo Kikuu cha Holon Institute of Technology nchini Israel na Chuo Kikuu cha Buraimi nchini Oman.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geofrey Pinda akijibu Swali Bungeni kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhusu Lugha ya Kiswahili inavyotoa fursa za ajira kwa Watanzania. 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.