Wednesday, October 12, 2022

TUENDELEE KUMUENZI MWALIMU NYERERE- MHE MAKINDA



Kamishna wa Sensa ya mwaka 2022 Mhe. Anne Makinda amewasihi Watanzania kuendelea kuenzi fikra na mitazamo ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Mhe. Makinda ametoa rai hiyo katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam alipofungua Kongamano la kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha Mwalimu Nyerere kilichotokea 1999 jijini London.

Amesema Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa muasisi wa vitu vingi ambavyo nchi yetu inajivunia hadi sasa, ni muasisi wa siasa za kutokufungamana na upande wowote, Ukombozi wa nchi za Bara la Afrika hasa zile za Kusini pamoja na kutokukubaliana na fikra za ukoloni na ubaguzi wa aina yoyote na kusisitiza kuwa ni lazima tuendelee kumuenzi kwa mambo makubwa aliyotufanyia

“Mwalimu alikuwa muasisi wa vitu vingi ambavyo nchi yetu inajivunia hadi sasa, alikuwa muasisi wa siasa za kutofungamana na upande wowote, kusimamia ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na kupinga ukoloni na ubaguzi wa aina yoyote ile, haya mambo ni makubwa sana lazima tuendelee kuyaenzi kwa nguvu zote,” alisema.

Amefafanua kuwa Hayati Mwalimu alitamani kuchelewesha uhuru wa Tanganyika kutokana na imani yake ya ukombozi wa nchi zote za Afrika kwakuwa aliona ukombozi wa mmoja hauna maana kama nchi nyingine hazitakuwa huru.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga amewashukuru watoa mada na washiriki wa kongamano hilo kwa michango yao ambayo imefanya kongamano hilo kufanikiwa na kutoa elimu kwa wengi.

“Watoa mada wetu wamesema mengi ya muhimu sana na tumejifunza kwa kina. Nawashukuru wote kwa mawasilisho yenu muhimu katika kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambalo limetukumbusha mambo mengi yaliyofanywa na Hayati Mwalimu Nyerere,” alisema Balozi Mindi.

Balozi Mindi pia amekipongeza Chuo cha Diplomasia kwa kuandaa Kongamano hilo kwa ajili ya kukumbuka miaka 23 tangu kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na hivyo kuwakutanisha wadau mbalimbali na kuwakumbusha, kujadili na kujifunza mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika Kujenga Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia ya Tanzania.

Kongamano hilo lilijadili mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika Kuendeleza Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia nchini liliwakutanisha mabalozi wastaafu na wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia na wanafunzi wa shule ya Sekondari Jitegemee ya Dar es Salaam.







No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.