Sunday, October 2, 2022

TANZANIA, KOREA KUIMARISHA MISINGI YA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Korea ili kuimarisha zaidi misingi ya uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizo.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) katika maadhimisho ya siku ya kuanzishwa kwa Taifa hill iliyofanyika  Jijini Dar es Salaam tarehe 1 Oktoba, 2022.

Mhe. Waziri Mulamula aliongeza kuwa Tanzania imekusudia kuendelea kuimarisha misingi ya uhusiano wake wa kidiplomasia uliopo kati yake na Jamhuri ya Korea kwa kuongeza maeneo ya ushirikiano katika sekta za maji, teknolojia, afya, elimu, nishati, usafirishaji na uchukuzi, pamoja na biashara na uwekezaji. 

“Mwaka huu tunatimiza miaka 30 ya uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati yetu, kudumu kwa ushirikiano huu muda wote ni ishara ya uhusiano mzuri uliopo baina yetu, tutaendelea kuulinda na kuuthamini ushirikiano huu nyakati zote kwa maslahi mapana ya nchi zetu mbili,” amesema Mhe. Balozi Mulamula

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri Mulamula ameongeza kuwa Jamhuri ya Korea imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Ameongeza kuwa, Wakala wa Kukuza Biashara na Uwekezaji wa Korea (KOTRA), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA) pamoja na Benki ya EXIM ya Korea ni Taasisi ambazo zinashiriki katika harakati za kuchangia maendeleo ya Taifa la Tanzania.

Naye Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini, Mhe. Kim Sun-Pyo amesema Tanzania imekuwa mdau mkubwa wa Jamhuri ya Korea kwa nyakati zote na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

“Tumekuwa tukishirikiana katika nyanja mbalimbali kama vile nishati, elimu, afya, maji na miundombinu hivyo ni matarajio yetu kuwa tutaendelea kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano hususan katika nyanja za biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa mataifa yetu,” amesema Mhe. Balozi Sun-Pyo.

Mhe. Balozi Sun-Pyo amesema takwimu za biashara zinaonesha kuwa ujazo wa biashara kati ya Korea na Tanzania umeongezeka lakini bado tumekusudia kuongeza maeneo ya ushirikiano ili kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wa mataifa yote mawili kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika mataifa haya.

Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha misingi ya uhusiano wa muda mrefu uliopo kati yake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akitoa hotuba yake ya ufunguzi wakati wa maadhimisho ya siku ya kuanzishwa kwa Taifa hill iliyofanyika  Jijini Dar es Salaam tarehe 1 Oktoba, 2022

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akitoa hotuba yake ya ufunguzi wakati wa maadhimisho ya siku ya kuanzishwa kwa Taifa hill iliyofanyika  Jijini Dar es Salaam tarehe 1 Oktoba, 2022








No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.