Wednesday, September 7, 2022

WAZIRI MULAMULA AKUTANA NA MABALOZI WA UTURUKI, ETHIOPIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) kwa nyakati tofauti amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Dkt. Mehment Gulluoglu na Balozi wa Ethiopia nchini, Mhe. Shibru Mamo Kedida tarehe 7 Septemba 2022 katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. 

Akiongea na Dkt. Gulluoglu Waziri Mulamula amesema  Tanzania itaendelea kushirikiana na Uturuki katika masuala ya biashara, masoko, kilimo, uwekezaji, utalii, madini na uchumi wa bluu.

Naye Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Dkt. Mehment Gulluoglu ameeleza kuwa katika kipindi chake cha uwakilishi anafanya jitihada za makusudi kuhakikisha Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki unafanyika ili kuongeza nguvu ya utekelezaji katika maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa.

Katika tukio jingine, Waziri Mulamula amemhakikishia Balozi wa Ethiopia nchini, Mhe. Kedida kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu na wa kihistoria ulioasisiwa na waasisi wa mataifa yao ili kufikia malengo ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Ameongeza kuwa Tanzania itaendelea kuzingatia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa katika Umoja wa Afrika hususan umuhimu wa mto Nile na manufaa yake katika sekta za kilimo na huduma nyingine za kijamii.

Naye Mhe. Kedida amemueleza Waziri Mulamula kuwa Ethiopia itaendeleza jitihada za kukuza ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo kusimamia makubaliano yaliyoanzishwa kati ya Tanzania na Ethiopia hususan ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji la Tanzania na Shirika la Utangazaji la Ethiopia pamoja na ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Ethiopia.

=======================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Dkt. Mehment Gulluoglu tarehe 07 Septemba 2022 katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na maafisa kutoka Wizara hiyo wakifuatilia mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Dkt. Mehment Gulluoglu katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Picha ya pamoja
==================================

Wakati huohuo Waziri Mulamula alikutana kwa mazungumzo na Balozi wa Ethiopia nchini, Mhe. Shibru Mamo Kedida.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Ethiopia nchini, Mhe.Shibru Mamo Kedida katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiteta jambo na Mhe. Kedida katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.