Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kusimamia mifumo ya utendaji kazi katika Serikali yake ili kuwawezesha wanawake na vijana washiriki kikamilifu katika biashara.
Ahadi hiyo imetolewa wakati wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara ulioandaliwa na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) na kufanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022.
Akiongea katika mkutano huo, Mhe. Rais Samia ameeleza baadhi ya maeneo ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imeyafanyia maboresho ili biashara zinazofanywa na Wanawake na Vijana nchini zilete matokeo chanya sambamba na kuinua kipato chao na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Maeneo hayo ni pamoja na: Kuondoa vikwazo vya biashara, kuwawezesha wanawake kupata mikopo ya riba nafuu, maboresho katika mifumo ya tozo katika sekta mbalimbali kama vile kilimo na madini, kuwezeshwa kupata vyeti vya ubora kwa ajili ya kuingia katika ushindani wa soko la kimataifa na kupunguza ushuru unaotozwa na mamlaka mbalimbali za Serikali.
Aidha, Mhe, Rais Samia amesema kuwa Serikali yake inatoa nafasi za upendeleo kwa sekta binafsi kushiriki katika shughuli za maendeleo, na kwa sasa Tanzania imetoa kipaumbele kwa wanawake ambapo asilimia 30 ya manunuzi yote makubwa ya Serikali yanatolewa kwa makampuni ya wanawake.
“Mapema mwezi Mei 2022 nikiwa nchini Ghana kwenye mkutano ulioratibiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Ghana ambao uliwakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali nilipewa heshima ya kuwa kinara wa hamasa ya kuinua Wanawake na Vijana kwenye biashara, hivyo naahidi kuendelea kusimamia mapambano hayo”. Alisema Mhe. Rais Samia.
Akieleza zaidi, Mhe. Rais Samia ameeleza kuwa ili kufikia malengo ya kuinua biashara ni vema sasa nchi za Afrika zikawekeza kwenye miundombinu ili ziweze kufikika na kurahisisha shughuli za biashara kwa wananchi wake ambapo sehemu kubwa ya wajasiliamali wake ni wanawake na vijana.
Pia amesisitiza kuwa manufaa ya itifaki ya Wanawake na Vijana katika biashara kwenye Mkataba wa Eneo Huru Barani Afrika hayawezi kupatikana moja kwa moja kama mipango ya kitaifa ya nchi wanachama haitowajumuisha wanawake na vijana katika utekelezaji wake.
Hivyo, ni vema nchi wanachama zikawekeza pia kwenye tafiti ili kufahamu namna bora ya kuondoa changamoto kwenye uhalisia wa jambo husika ambapo alieleza kwa nyakati tofauti Tanzania imefanya tafiti katika masoko ili yaweze kunufaisha wanawake na kusaidia kuwajengea miundombinu wezeshe kwa shughuli za biashara.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais ameeleza kuwa Tanzania inaandaa mpango wa kusimamia usawa kwa kizazi kijacho ili kuwawezesha wanawake kupata fursa sawa na wanaume na kuhakikisha wanawake na vijana wanawezeshwa kiuchumi na kuwekewa mfumo utakaowawezesha kupata ajira rasmi na zenye ujira utakaowainua kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa.
Mhe. Rais Samia pia alitumia fursa ya mkutano huo kunadi fursa za uwekezaji zilizopo nchini katika sekta za kilimo cha mazao ya chakula, matunda na mbogamboga, sekta ya mifugo hususan nyama na bidhaa za ngozi, madini na utalii.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Mhe Balozi Liberata Mulamula katika mkutano huo aliongoza majadiliano yaliyokuwa na mada isemayo “Kuunga mkono Uongozi wa Wanawake na Vijana katika Biashara” (Supporting Women and Youth’s Leadership in Trade).
Mjadala huo ulihusisha viongozi wakuu wanawake wa nchi za Afrika ambao ni: Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Joyce Banda, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Liberia, Mhe. Dkt. Jewel Taylor-Howard, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Jessica Allupo, Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika,Mhe. Wamkele Mene na Naibu Mwenyekiti, Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Dkt. Monique Nsanzabaganwa.
Washiriki wengine wa mkutano huo ni pamoja na: Mabalozi, Mawaziri wanaohusika na Biashara na Mawaziri wanaohusika na masuala ya jinsia. wanawake na vijana wanaojishughulisha na masuala ya biashara, watunga serĂ¡ na wadau wa maendeleo.
Sanjari na mkutano huo, wajasiriamali zaidi ya 80 wameshiriki kwenye maonesho ya bidhaa mbalimbali ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina washiriki wapatao 72.
==============================================================
Sehemu ya Mawaziri na Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara kwenye Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) unaofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (JNICC) Jijini Dar es Salaam. |
|
Katibu wa Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Bw. Seif Kamtunda akifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara kwenye Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) unaofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (JNICC) Jijini Dar es Salaam. |
Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Jessica Allupo akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara kwenye Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) unaofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (JNICC) Jijini Dar es Salaam. |
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akisherehesha wakati wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara kwenye Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) unaofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (JNICC) Jijini Dar es Salaam. |
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akisalimiana na sehemu ya Mawaziri walioshiriki Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara kwenye Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) unaofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (JNICC) Jijini Dar es Salaam. |
Picha ya pamoja |
Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiongoza majadiliano yaliyokuwa na mada isemayo “Kuunga mkono Uongozi wa Wanawake na Vijana katika Biashara” (Supporting Women and Youth’s Leadership in Trade) wakati wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara kwenye Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) unaofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (JNICC) Jijini Dar es Salaam. |
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Joyce Banda akichangia hoja kwenye majadiliano yaliyokuwa na mada isemayo “Kuunga mkono Uongozi wa Wanawake na Vijana katika Biashara” (Supporting Women and Youth’s Leadership in Trade) wakati wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara kwenye Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) unaofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (JNICC) Jijini Dar es Salaam. |
Majadiliano yakiendelea. |
Picha ya pamoja, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Joyce Banda (wa pili kushoto) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Liberia, Mhe. Dkt. Jewel Taylor-Howard (wa pili kulia), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Jessica Allupo (katikati) na Naibu Mwenyekiti, Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Dkt. Monique Nsanzabaganwa (wa kwanza kushoto). |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.