Mawaziri wa kisekta wa Serikali za Tanzania na Afrika Kusini
wamekutana jijini Pretoria, Afrika kusini kushiriki Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja
ya Ushirikiano (Bi-National Cooperation - BNC) ngazi ya Mawaziri kati ya nchi
hizo uliofanyika tarehe 15 Machi 2023.
Mkutano huu wa siku moja ulitanguliwa na mkutano ngazi ya
wataalamu uliofanyika tarehe 13 na 14 Machi 2023 ambao pamoja na mambo mengine
ulikuwa na jukumu la kuandaa taarifa kwa ajili ya mkutano wa ngazi ya Mawaziri.
Mkutano wa Mawaziri umepitia na utawasilisha taarifa katika
itakayojadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika mkutano wa Wakuu wa Nchi hizo
unaotarajiwa kufanyika tarehe 16 Machi 2023.
Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ngazi ya Mawaziri
ulifunguliwa kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Mwenyekiti mwenza Waziri wa
Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor
ambao wameongoza ujumbe wa nchi hizo mbili katika mkutano huo.
Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Dkt. Tax ameeleza kuwa Mkutano
wa Pili wa Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini unaonesha nia
ya dhati ya mataifa hayo ya kuendeleza ushirikiano wa kihistoria na kidiplomasia
uliopo.
“Mkutano huu unatoa fursa ya kujadili na kuamua masuala ya
msingi ya kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya nchi na watu kupitia muingiliano
uliopo katika shughuli mbalimbali za kijamii, biashara na uwekezaji” alisema
Dkt. Tax
Pia akaeleza mkutano huo wa BNC utaweka msisitizo katika masuala
ya ustawi wa jamii wa mataifa hayo mawili pamoja na watu wake.
Mkutano huo utajadili masuala ya ushirikiano yenye tija kwa nchi
hizo na kupelekea maamuzi yatakayoleta matokeo chanya na kutoa ufumbuzi wa changamoto
za wananchi.
Dkt. Tax amesema sekta binafsi ni chachu katika kuendesha uchumi
wa nchi, pia ni wadau muhimu kwa sekta za umma hivyo ni jukumu la Serikali
kuwezesha upatikanaji wa mazingira mazuri ya biashara ili ziweze kukuza uchumi wa
nchi.
Kwa upande wa Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa
Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Nalendi Pandor ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania
na Afrika kusini umejengwa na historia yenye uhalisia iliyoasisiwa tangu enzi
za harakati za kupinga ubaguzi wa rangi pamoja na za ukombozi wa Kusini mwa
Afrika.
Ameongeza kuwa Afrika Kusini itaendelea kushirikiana na Tanzania
hususan katika shughuli za kijamii, kiuchumi na masuala ya kiutamaduni.
“Napongeza jitihada za mshikamano zilizooneshwa na
wafanyabiashara wa Afrika Kusini na Ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania
kwa kusaidia madawati 400 katika shule za Wilayani Kongwa na vifaa wezeshi vya
usafi katika shule ya miyembeni mwaka 2018” alisema Dkt. Pandor.
Aidha, akaeleza kuwa Tanzania na Afrika Kusini zina matamanio
makubwa ya kukuza uchumi utakaotengeneza ajira na kuondoa umasikini na kujenga
usawa wa hali ya kimaisha kwa wananchi wake.
Vilevile, Tanzania na Afrika Kusini zina mtazamo unaofanana
katika masuala ya usalama, uchumi na misimamo ya kimaendeleo ya kikanda na
kimataifa hivyo, BNC ni sehemu ya jitihada zitakazowezesha kuongezeka kwa miradi
ya maendeleo na mshikamano imara utakaopelekea kukuza na kuimarisha ushirikiano
uliopo.
Mkutano wa BNC unajadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa
katika sekta mbalimbali za ushirikiano zilizokubaliwa na nchi hizo. Sekta hizo
ni pamoja na; Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Fedha na Uchumi, Nishati, Mifugo na Uvuvi, Madini, Habari, Mawasiliano
na teknolojia ya mawasiliano, Kilimo, Uchukuzi, Elimu na Mafunzo, Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Utalii, Maji na Misitu, na Afya.
Kwa pamoja viongozi hao walizitaka sekta zilizopo katika maeneo
hayo ya ushirikiano kuhakikisha wanatekeleza na kutatua kwa wakati masuala ya
kiutendaji ili kuruhusu sekta hizo kustawi kiuchumi na kuyafikiwa kwa wakati
malengo ya Wakuu wa Nchi katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania na Afrika
Kusini.
Mkutano huu unaenda sambamba na kongamano la biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini litakaalofanyika tarehe 16 Machi 2023 na kuhusisha maonesho ya huduma na biashara kutoka sekta za umma na sekta binafsi ambapo washiriki wapatao 136 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano na maonesho hayo jijini Pretoria, Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.