Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imefungua rasmi Ofisi za Ubalozi jijini Windhoek, Namibia.
Hafla ya ufunguzi wa ofisi
hizo za ubalozi ulihudhuriwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Mabalozi wa nchi za Afrika, viongozi wa
Serikali ya Tanzania na viongozi wa jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini
humo.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Waziri Dkt. Tax ameishukuru Jamhuri ya Namibia hususan Wizara ya Mambo ya
Nje kwa ushirikiano ilioutoa katika hatua zote za kuanzisha ofisi hiyo na
kuelezea kuwa kushiriki kwao katika tukio hilo la kihistoria la ufunguzi ni
hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo.
Amesema Tanzania
kama mama wa lugha ya Kiswahili inaendelea na jitihada za
kuhakikisha lugha hiyo inatangazwa na kuenea kwa kasi kupitia Balozi zake, vyuo
vya kimataifa na majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
“Wakati huu ambapo Serikali
za Tanzania na Namibia zipo kwenye mazungumzo ya lugha ya Kiswahili kuwa sehemu
ya lugha ya chaguo katika shule za Namibia, Ubalozi umefungua maktaba ndogo
yenye vitabu na majarida ya Kiswahili kwa ajili ya watu wenye nia ya kujifunza
kiswahili kuja kujisomea” alisema Dkt. Tax
Naye Mhe. Dkt. Ndaitwah
akizungumza katika hafla hiyo alieleza kuwa kwasasa nchi hizo mbili zina makazi
ya ubalozi katika miji mikuu ambapo ni hatua muhimu katika kukuza na kuimarisha
ushirikiano baina ya nchi hizo na watu wake.
Kadhalika, amempomgeza
Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba kwa kuchagua
jengo lenye ubora na la kisasa kwa ajili ya ofisi za ubalozi huo ambalo ni
rafiki kwa mazingira.
‘’ Tanzania ikiwa
mpambanaji wa bara la Afrika na Kusini mwa Afrika siku zote imekuwa pamoja nasi
na hivyo sisi wanamibia tutakapokuja kujisomea na kufanya tafiti katika maktaba
hii ya Kiswahili inayofunguliwa leo tutakuwa katika mazingira salama” alisema
Mhe. Ndaitwah.
Ubalozi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania nchini Namibia ulianza utekelezaji wa majukumu yake ya
kidiplomasia tarehe 20 Februari 2020 na kufanya Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba
kuwa Balozi wa kwanza kuwaiwakilisha Tanzania katika nchi hiyo.
Hafla ya ufunguzi wa
Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia imefanyika pembezoni
mwa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na
Namibia unaofanyika jijini Windhoek Namibia kuanzia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023
ambapo Mhe. Dkt. Tax anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo.
Wakati huo huo, Waziri Dkt.
Tax alifanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini
Namibia ambao walijitambulisha kitaaluma ni Madaktari wa Binadamu.
Pamoja na mambo mengine
Mhe. Waziri aliwasihi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania wanapokuwa nje
ya nchi na kuendelea na zoezi la kujiandikisha linalofanyika kwa watanzania
wenye taaluma mbalimbali waliopo nje ya nchi ili waweze kutambulika na
kuisaidia nchi yao katika taaluma hizo pale wanapohitajika.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.