Saturday, July 9, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA NSSF ZAJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI NJE YA NCHI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii - NSSF, Bw. Masha Mshomba tarehe 8 Julai 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.


Viongozi hao wamejadili juu ya umuhimu wa kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya Wizara na mfuko huo wa NSSF.  


Pamoja na mambo mengine viongozi hao wamezungumzia kuhusu uwekezaji kwenye viwanja vya Serikali nje ya nchi ili kuona namna ambavyo Wizara na NSSF wanaweza kushirikiana katika miradi ya ujenzi wa ofisi na vitega uchumi.


Aidha, Balozi Sokoine akaeleza kuwa Serikali ina miliki viwanja zaidi ya 40 kwenye maeneo ya uwakilishi nje ya nchi, hivyo akatoa rai kwa taasisi hiyo kushirikiana na Wizara katika kuviendeleza kwa kujenga majengo ya Ofisi za Balozi pamoja na vitega uchumi ili kuipunguzia Serikali gharama ya kupanga lakini zaidi  kupata faida kutokana na vitega uchumi hivyo.


Naye Bw. Mshomba aliafiki wazo hilo la uwekezaji na kueleza kuwa  NSSF imeshakuwa na mipango ya miradi ya uwekezaji nje ya nchi hivyo, wazo hilo limekuja wakati mwafaka na kwamba NSSF inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kufungua mipaka hususan katika sekta ya biashara na uwekezaji.


Aidha, Kikao hicho kiliridhia kuundwa kwa timu ya Wataalamu kutoka katika pande zote mbili ili kuruhusu kufanyika kwa tathmini ya kina juu ya uwekezaji huo na faida zake ili kuweza kuwa na miradi ya pamoja na Wizara wenye tija kwa Taifa.


======================================


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Joseph Sokoine (kulia) amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii - NSSF, Bw. Masha Mshomba tarehe 8 Julai 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii - NSSF, Bw. Masha Mshomba (wa pili kulia) akiwa katika mazungumzo na Balozi Joseph Sokoine (hayupo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
 Kulia ni Mkurugenzi wa Mipango na Utawala - NSSF, Bw. Gabriel Silayo na wa tatu kutoka kulia ni Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma - NSSF, Bi. Lulu Mengele.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango, Bw. Justin Kisoka akifafanua juu ya uwekezaji wa miradi ya pamoja na namna Wizara na NSSF zinavyoweza kushirikiana katika kutathmini uwekezaji kwenye maeneo ya miradi.

Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana na kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara hiyo wakifuatilia mazungumzo.

Picha ya pamoja

 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.