Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa rai kwa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuweka jitihada za makusudi za
kukikuza Kiswahili nje ya mipaka ya Tanzania.
Rai hiyo imetolewa wakati wa
sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa Leo
tarehe 7 Julai 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mpango akiwa Mgeni Rasmi
katika maadhimisho hayo ameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki imeendelea kubeba jukumu la kizalendo ambapo, kupitia Balozi
zake ilifanikiwa kushawishi majukwaa ya kimataifa kuitambua lugha ya Kiswahili
na kupewa siku ya kuadhimishwa duniani ambayo inafanyika leo kwa mara ya
kwanza.
“Ninatoa pongezi kwa Balozi
zetu kwa jitihada wanazofanya za kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili, nimeona
mitandaoni jinsi Balozi zilivyojitoa kufanya makongamano na midahalo ya
Kiswahili katika kusherehesha siku hii” alisema Mhe. Mpango.
Pamoja na kutolewa kwa pongezi
kwa Wizara, Mhe. Mpango ametoa pongezi za kipekee kwa Mabalozi wa Tanzania
wanaowakilisha Jijini New York, Marekani, Mhe. Kennedy Gaston; Addis Ababa,
Ethiopia, Mhe. Innocent Shio na Paris, Ufaransa, Mhe. Samuel Shelukindo kwa
kukamilisha mchakato wa kutambulika kwa Kiswahili duniani.
Aidha, uwepo wa siku maalum ya
kuadhimishwa lugha ya Kiswahili duniani kukupa nguvu ikiwa ni lugha rasmi ya
kazi katika Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kufanya jumuiya nyingine ambazo
Tanzania ni mwanachana kuipa upekee lugha ya Kiswahili.
Naye Balozi wa Tanzania nchini
Ethiopia na Mwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Innocent
Shio ameeleza kuwa lugha ya Kiswahili ina nafasi kubwa katika kukuza na
kuimarisha mtangamano kwa maendeleo ya Afrika kwakuwa, mawasiliano huleta amani
na kuongeza mshikamano.
Pia, akaeleza wakati huu
ambapo Umoja wa Afrika unaenda kutathmini Agenda 2030 na kutekeleza kikamilifu
Agenda 2063 ya Umoja huo ni wakati sasa wa kukibidhaisha kiswahili ili
kuunganisha mataifa ya Afrika na kuweza kuyafikia malengo ya mpango wa Eneo
Huru la Biashara la Afrika (AfCTA) katika kukuza sekta za kiuchumi na kuinua
pato la Wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Lugha ni bidhaa hivyo ni
muhimu kusimamia kikamilifu soko lake ili kuleta fursa zinazotarajiwa, mathalan
ajira kwa Walimu, Wakarimali, huduma ya kutafsiri, utangazaji, uandishi wa
vitabu vya Kiswahili, Sanaa ya uigizaji na uhariri” alisema Balozi Shio.
Tarehe 23 Novemba 2021,
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza
Siku Maalumu ya Kiswahili Duniani inayoadhimishwa tarehe 7 Julai kila mwaka.
Sherehe za maadhimisho ya Siku
ya Kiswahili Duniani, zimeandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na
kuhudhuriwa na Viongozi wa Wizara, Taasisi, Idara, sekta binafsi na taasisi ya
za elimu nchini na Wananchi.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.