Wednesday, July 20, 2022

MKUTANO WA KAMATI YA MAWAZIRI WANAOSHUGHULIKIA URATIBU NA UDHIBITI WA MAAFA WAFANYIKA MALAWI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene (Mb.), ameongoza ujumbe wa wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wanaoshughulika na Uratibu na Udhibiti wa Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 19 Julai, 2022, Lilongwe, Malawi.


Mkutano huu pamoja na masuala mengine, ulijadili agenda kuhusu Uendeshaji wa Kituo cha Operesheni za Dharura na huduma za Kibinadamu cha SADC na kuhimiza Nchi Wanachama kukamilisha michakato ya ajira za kushikiza ili Kituo hicho kiweze kupata watumishi wa kutosha ili kukiwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Akichangia hoja katika agenda hii, Mhe. Simbachawene aliipongeza Sekretarieti ya SADC kwa jitihada mbalimbali zinazotekelezwa na pia alishauri kuwa Sekretarieti ya SADC iangalie njia mbalimbali za kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuimarisha utendaji kazi wa Kituo hicho.

Mkutano huu wa Mawaziri ulitanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu wa Kamati ya Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Uratibu na Uthibiti wa Maafa, kilichofanyika tarehe 17 Julai 2022. Meja Jenerali Michael  Mumanga, Mkurugenzi wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu - Idara ya Maafa, aliongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Kikao hicho. Pamoja nae aliambatana na Afisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Maafa, Afisa Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Hali ya Hewa na Afisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene (wa pili kushoto), ameongoza ujumbe wa wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wanaoshughulika na Uratibu na Udhibiti wa Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 19 Julai, 2022, Lilongwe, Malawi. Pichani Mhe. Simbachawene akiwa katik apicha ya pamoja na Wajumbe kutoka Nchi za SADC walioshiriki mkutano huo.

Picha ya pamoja

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.