Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Jen. Evariste Ndayishimye amekabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta wakati wa Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika tarehe 22 Julai 2022.
Akikabidhi
nafasi hiyo Mhe. Kenyatta aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya
jumuiya hiyo wakati wa uongozi wake ambapo alieleza kwamba Jumuiya imefanikiwa
kukamilisha mchakato wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa mwanachama,
Kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara 13 kati ya 22 vilivyokuwepo awali,
kutafuta ufumbuzi wa pamoja katika changamoto za Covid–19 na kuanzisha mchakato
utakaowezesha nchi wanachama kupata chanjo ya Covax.
Masuala
mengine ya utekelezaji ni; Kuhakikisha Burundi inafanikiwa kushiriki katika Shirikisho
la Afrika Mashariki, kusimamia ushiriki wa asasi za kiraia na ushiriki wa sekta
binafsi katika utekelezaji wa majukumu ya kikanda.
Naye
Rais wa Burundi, Mhe. Jen. Ndayishimye baada ya kupokea majukumu hayo ya nafasi ya
Mwenyekiti, alimshukuru Mhe. Kenyatta kwa uongozi bora na kwa mafanikio
yaliyopatikana katika uongozi wake.
Aidha,
akazishukuru nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kwa kuiamini Burundi kuongoza, na
akaeleza uelekeo wa utekelezaji wa majukumu katika kipindi chake cha uongozi utazingatia
masuala yafuatayo; Kukuza mtangamano wa Afrika Mashariki na kuimarisha ujirani
mwema; kuharakisha mkakati wa viwanda katika Jumuiya; Kuzingatia ombi la
Jamhuri ya Shirikisho la Somalia kujiunga na Jumuiya hiyo na Usimamizi wa
agenda ya amani na usalama ili kuondoa migogoro.
Masuala
mengine yatakayosimamiwa ni pamoja na; Kuimarisha mfumo wa mageuzi ya
kitaasisi, Kuendelea kusisitiza umuhimu wa maridhiano ya kitaifa ili kuweza
kuyafikia maridhiano ya kisiasa katika ngazi ya jumuiya, Ushirikishwaji wa
Wanawake na Vijana; na Wake za viongozi kushirikishwa katika utekelezaji wa
malengo ya jumuiya.
Naye
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia katika mkutano huo alimuaga Mhe. Kenyatta kwakuwa anaelekea kipindi cha mwisho
cha uongozi wake nchini Kenya kuitakia nchi hiyo uchaguzi mkuu mwema
unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2022.
Pamoja
na mambo mengine mkutano huo umemchagua Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru
Kenyatta kuwa msimamizi wa mazungumzo ya amani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC); umefanya uapisho wa majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki ambao
ni; Mhe. Jaji Leonard Gacuko kutoka Burundi na Mhe. Jaji Cheborion Barishaki
kutoka Uganda.
Pia
mkutano huo ulikabidhi zawadi kwa wanafunzi wa sekondari walioshinda katika
nafasi mbalimbali kwenye mashindano ya uandishi wa insha kwa lugha ya Kiswahili, kiingereza na kifaransa. Walishiriki hao ni wale ambao walishiriki mashindano hayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021 lakini hawakukabidhiwa zawadi
kufuatia kutoitishwa kwa mikutano ya Wakuu wa Nchi ya ana kwa ana kutokana na
changamoto ya maambukizi yaCovid-19.
===========================================
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.