Friday, May 28, 2021

WAZIRI MULAMULA AHIMIZA KASI NA WELEDI KATIKA UTENDAJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mkutano na watumishi wa Wizara jijini Dodoma. Pamoja na mambo mengine mkutano huu ulilenga kutoa maelekezo kwa watumishi wa Wizara ili kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi, pia kusikiliza changamoto mbalimbali kutoka kwa Watumishi ili kuzipa suluhisho la kudumu.  

Waziri Mulamula ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha na kuwahimiza watumishi wa Wizara kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kujituma ili kukidhi matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita na Watanzania kwa ujumla. “Watanzania wanamatarajio makubwa na Wizara yetu, tunajukumu kubwa la kuhakikisha tunatimiza matarajio yao hivyo ni lazima tufanye kazi kwa kujituma na weledi zaidi, pia kuacha kufanya kazi kwa mazoea” Waziri Mulamula. 

Aidha, Waziri Mulamula ameeleza dhamira yake ya kuhakikisha kuwa Wizara inatafuta fursa mbalimbali za masomo ya muda mfupi na mrefu ili kuwaongezea ujuzi watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao. Sambamba na hilo, Waziri mulamula ameleza kuwa Wizara inadhamira ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi ili kuwaogezea hali katika utendaji. “Natambua kuwa ufanisi katika Wizara hii hauwezi kupatikana iwapo mazingira ya ufanyaji kazi sio mazuri. Kupitia kwa Katibu Mkuu, tuna dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi, kuhakikisha upandishwaji wa vyeo unakamilika na kuhakikisha kuwa watumishi wanapata stahili zao ipasavyo na kwa wakati” Waziri Mulamula

Kwa upande wake Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu wa Wizara amewasisitiza Watumishi kufanya kazi kwa ubunifu na kwa umoja ili kuendelea kukuza mahusiano ya kiuchumi na mataifa, jumuiya za kikanda na taasisi nyingine za kimataifa. Balozi Sokoine ameongezea kusema ni vyema watumishi wa Wizara kuendelea kuungana na kushirikiana vyema katika kulinda uchumi na masilahi mapana ya Taifa. Vilevile kuhakikisha kuwa balozi zetu zinakuwa kiungo muhimu cha kukuza uwekezaji na upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zetu.

Waziri Mulamula na Balozi Sokoine wamekutana na Watumishi wa Wizara kwa mara ya kwanza tokea walipoteuliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nyadhifa zao. Mkutano huu pia ulihusisha Ofisi za Balozi zinazoiwalikilisha Tanzania sehemu mbalimbali duniani ambao wameshiriki kwa njia ya mtandao. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Wizara. Wengine walioketi, ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Edward Sokoine (kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bw. Alex B.D.J Mfungo (kulia)


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea baina yake na Watumishi wa Wizara uliofanyika jijini Dodoma

Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Liberata Mulamula na Watumishi wa Wizara


Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano
Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza na watumishi (hawapo pichani) wakati wa Mkutano wa Waziri Mulamula na Watumishi wa Wizara

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.