Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amehitimisha ziara yake katika Mikoa inayopitiwa na mradi wa maendeleo wa kuboresha miundombinu ya Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Mtwara Corridor). Mradi huu unahusisha ujenzi wa bandari ya Mtwara (ambao unaendelea kwa kasi), ujenzi wa barabara katika kiwango cha lami kuanzia Bandari ya Mtwara hadi bandari ya Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma sambamba na ujenzi wa bandari hiyo.
Lengo la ziara hii ilikuwa ni kuangalia hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu ya bandari na barabara katika ushoroba huo, kufanya mazunguzmzo na viongozi wa Serikali za Mikoa na Wilaya, ambapo Mheshimiwa Ndumbaro alitumia nafasi hiyo kuhimiza Mamlaka za Mikoa na Wilaya, kulinda na kuboresha uhusinao wa kidipolomasia na nchi tunazopakana nazo katika ukanda huo ili kujenga mazingira rafiki ya kibiashara, wakati huu ambao Serikali ya Awamu ya Tano imeboresha miundombinu inayowezesha kuzifikia nchi hizo kiurahisi zaidi.
Ujenzi wa miundombinu katika Ukanda wa Kusini mwa Nchi unachochea ukuaji wa biashara katika ukanda huo kwa kurahishisha usafirishaji na mawasiliano na kuzifikia kiurahisi Nchi jirani za Malawi, Kaskazini mwa Msumbiji na Zambia.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Ndumbaro aliambatana na Balozi wa Malawi nchini Mhe.Glad Chembe Munthali, ambaye amefurahishwa na kuridhishwa na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga mazingira rafiki ya kibiashara na nchi jirani kwa kuboresha miundombinu inayoziwezesha nchi hizo kunufaika na huduma za bandari nchini kiurahisi na kwa gharama nafuu.
Kadhalika, nia ya Mhe. Munthali Balozi wa Malawi nchini, katika ziara hiyo ilikuwa ni kuangalia kwa namna gani wafanyabiashara kutoka nchini kwake watanufaika na uboreshwaji wa miundombinu ya ushoroba wa Mtwara katika kusafirisha bidhaa zao kwa muda mfupi na gharama nafuu.
Aidha, kwa nyakati tofauti Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius G. Byakanwa, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme na Mkuu wa Wilaya Nyasa Mhe. Isabela Chilluba wameelezea utayari wao wa kuratibu na kusimamia shughuli na fursa za biashara zinazotokana na maboresho ya miundombinu katika ukanda huo.
Ziara hii ni mwendelezo wa jitihada zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Mamlaka mbalimbali za ndani katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kukuza biashara na kuvutia uwekezaji nchini.
Ujenzi wa barabara ya Mtwara hadi bandari ya Mbamba Bay kwa kiwango cha lami unafikia ukingoni, mkandarasi anaendelea na ujenzi wa sehemu iliyosalia (Mbinga hadi Mbamba bay) ambapo anataraijia kukabidhi barabara hiyo Septemba, 2020.
Ujenzi wa miundombinu katika ushoroba wa Mtwara umeleta mapinduzi makubwa ya maendeleo ya uchumi na kijamii katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania sambamba na kuliongezea Taifa mapato.
Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na Watendaji wa Bandari ya Mtwara na Viongozi wa Mkoa alipotembelea eneo la bandari ya Mtwara |
Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na Mhe. Isabela Chilluba Mkuu wa Wilaya ya Nyasa alipowasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja |
Picha ya pamoja |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.